1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China: Hakuna kitisho kutoka Roketi inayorejea duniani

7 Mei 2021

China imesema Roketi inayorejea duniani kutoka kituo chake cha anga za mbali haiwezi kuwa na madhara.

Weltspiegel | China Rakete Langer Marsch 5B
Picha: Getty Images/AFP

Roketi hiyo aina ya Long March 5G iliyorushwa na China, imejiachanisha na kituo cha anga za mbali cha China na wataalamu wameonya kwamba inaweza kuanguka kwebye makazi ya watu na kusababisha maafa na uharibifu mkubwa.

Hata hivyo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Wang Wenbing amesema mamlaka za nchi hiyo zinafuatilia kwa karibu na zitatoa taarifa zaidi juu ya kuanguka kwa roketi hiyo inayotegemewa kuufikia uso wa dunia mwishoni mwa juma hili.

 "Kutokana na jinsi ninavyoelewa roketi hiyo inatumia mfumo maalum wa kiteknolojia utakaosababisha iungue na kuharibiwa wakati wa kuanguka, kwahiyo kuna uwezekano mdogo sana wa kusababisha uharifu kwenye usafiri wa anga na ardhini" alisema bwana Wang Wenbing.

Picha za kituo cha anga za mbali cha China Picha: Tingshu Wang/REUTERS

Kiwango kikubwa cha mabaki ya roketi hiyo yanategemewa kuanguka duniani siku ya Jumamosi katika sehemu ambayo haijulikani mpaka sasa. Kituo cha masuala ya anga cha China hakijasema chochote kama roketi hiyo ya Long March 5B itaanguka ikiwa inathibitiwa vilivyo au la.

Mwezi Mei mwaka jana roketi ya China ilianguka bila kudhibitiwa katika bahari ya Atlantiki upande wa karibu na Afrika Magharibi. Gazeti la kikomunisti la Global Times lilidai kwamba kiwango kikubwa cha kipande cha roketi hiyo kitaungua angani na kutosababisha hatari kubwa kwa watu.

Marekani ina wasiwasi na athari za Roketi hiyo

Kitengo cha ulinzi cha Marekani kinategemea kwamba roketi hiyo itaanguka duniani siku ya Jumamosi, lakini hakijui itaangukia sehemu gani. Hiyo itafahamika ndani ya masaa machache baada ya roketi hiyo kuingia duniani, kitengo hicho cha ulinzi cha Marekani kiliandika siku ya Jumane.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Jen Psaki Picha: Drew Angerer/Getty Images

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Jen Psaki alisema siku ya Jumatano kuwa kitengo maalum cha anga cha Marekani kinafahaumu kuhusu tukio hilo na kipo kwenye mkakati wa kufuatilia mahali ambapo roketi hiyo itaangukia.

Taasisi isiyo ya kiserikali ya Aerospace Corp iliyopo Marekani, inategemea kwamba mabaki ya roketi hiyo yataangukia karibu na bahari ya Pasifiki karibu na Equator baada ya kupita juu ya miji ya mashariki mwa Marekani.

Roketi hiyo ambayo inakadiriwa kuwa na takribani mita 30 itakuwa ni kati ya roketi zilizoanguka na kusababisha mabaki ya uchafu mkubwa duniani. Roketi yenye tani 18 ya China iliyoanguka mwezi Mei mwaka jana, ilikuwa ni kati ya roketi zilizoanguka na kusababisha uchafu mkubwa duniani.