China imerejelea vitisho vya kuishambulia Taiwan
11 Januari 2023Msemaji wa Ofisi ya China inayoshughulikia masuala ya Taiwan, Ma Xiaoguang, amesema nchi hiyo imejitolea tena mwaka huu kwa kile alichokitaja kama ''kulinda mamlaka na uadilifu wa eneo na kuvunja njama ya uhuru wa Taiwan" katika kisiwa hicho kinachojitawala kidemokrasia tangu kilipojitenga kutoka kwa China mwaka 1949.
soma Kiongozi wa Taiwan aiambia China vita sio chaguo
China inaiona Taiwan kama eneo lake ambalo lazima liwe chini ya udhibiti wa Beijing, hata kwa kutumia nguvu ikiwa italazimika. Msururu wa ziara katika miezi ya hivi karibuni ya wanasiasa wa kigeni kisiwani Taiwan, ikiwa ni pamoja na ya Spika wa Bunge la Marekani Nancy Pelosi na wanasiasa wengi kutoka Umoja wa Ulaya, ulichochea majaribio ya nguvu za kijeshi kutoka pande zote mbili.
Wiki hii, wanajeshi wa Taiwan wanaendelea na mazoezi yanayokusudiwa kuhakikishia umma uwezo wake wa kukabiliana na vitisho vya China wakati wa likizo ya Mwaka Mpya katika tamaduni ya China.
Mazoezi hayo yanaambatana na ziara ya wabunge wa Ujerumani na Lithuania, taifa la Baltic ikiwa shabaha maalum ya China yenye hasira kwa kuboresha uhusiano wake na Taiwan.
Umuhimu wa kuepusha mvutano
Ujumbe wa wabunge wa Ujerumani nchini Taiwan umezungumzia juu ya umuhimu na wajibu wa kimaadili ili kuepusha kuongezeka kwa mvutano katika Ujia wa Bahari wa Taiwan.
Johannes Vogel, makamu mwenyekiti wa Chama cha Free Democratic nchini Ujerumani amesema "Kuna wajibu wa kimaadili, nadhani, kwa kila mtu kuepuka uvamizi wa kijeshi katika Ujia wa Bahari wa Taiwan. Na kisha, mtu lazima afikirie ni nini unaweza kuleta kwenye meza ya mazungumzo na tunafikiria njia ya kuzuia hali mbaya ya kiuchumi, jambo ambalo sisi tunaweza kuleta mezani."
soma Taiwan yaanza mazoezi ya ufyatuaji mizinga
Kiongozi wa chama cha SPD cha Ujerumani Lars Klingbeil ameliambia gazeti la kila wiki la Ujerumani, Die Zeit katika maoni yaliyochapishwa leo Jumatano kwamba Ujerumani italazimika kukata uhusiano na China kama ilivyo na Urusi ikiwa China itaishambulia Taiwan.
Ujerumani inafanyia kazi mkakati mpya wa China ambao unachukua zaidi mtazamo mzuri wa mahusiano na inalenga kupunguza utegemezi kwa nguvu kubwa ya kiuchumi barani Asia.
Juhudi za China kukitenga kisiwa hicho kidiplomasia zimeiwacha Taiwan na washirika 14 rasmi wa kidiplomasia, ingawa inasalia na uhusiano thabiti usio rasmi na mshirika mkuu, Marekani na zaidi ya mataifa 100 duniani kote.
AP//Reuters