1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
AfyaAsia

China yashuhudia ongezeko la magonjwa ya mfumo wa upumuaji

Angela Mdungu
29 Novemba 2023

Msimu wa mafua na homa umeshika kasi China, picha za hospitali zilizofurika wagonjwa na kumbukumbu za muitikio dhaifu katika kuchunguza chanzo cha UVIKO, vimeifanya dunia ifuatilie kwa karibu kinachoendelea nchini humo.

Hospitali ya watoto ya Peking
Watoto na wazazi wakisubiri huduma katika hospitali ya watoto mjini BeijingPicha: Jade Gao/AFP

Wiki iliyopita, Shirika la afya duniani, WHO liliitaka China itoe taarifa wakati kukiwa na wasiwasi wa ongezeko la maradhi ya mfumo wa upumuaji kwa watoto. Ongezeko hilo limeshuhudiwa hasa katika maeneo ya kaskazini ambayo shirika hilo limekuwa likiyafuatilia tangu mwezi Oktoba.

Soma zaidi: China yasema ongezeko la magonjwa ya kupumua linatokana na mafua na vimelea vya kawaida

Katika mkutano wa dharura kwa njia ya video uliofanyika Alhamisi iliyopita, maafisa wa afya wa China waliiambia WHO kwamba, magonjwa hayo yamesababishwa na "vimelea vya kawaida" na yanawapata watoto.

Kulingana na ripoti ya shirika hilo iliyotolewa baada ya mkutano huo, vimelea hivyo ni pamoja na vya homa ya mafua, virusi vinavyosababisha matatizo ya upumuaji vinavyojulikana kama RSV pamoja na bakteria wanaosababisha ugonjwa wa homa ya mapafu.

Soma zaidi: WHO: China watoe data ya ongezeko la maradhi ya kupumua

Vimelea hivyo vimekuwa vikisambaa China kwa wiki kadhaa sasa. Ripoti hiyo imeongeza kuwa, maafisa wa afya wameeleza kwamba kuongezeka kwa magonjwa ya mfumo wa upumuaji hakujasababisha kuwepo wagonjwa wengi wanaozidi uwezo wa hospitali za nchi hiyo.

Misururu ya wagonjwa waliojawa na wasiwasi hospitalini

Hata hivyo, katika wiki kadhaa zilizopelekea Shirika la afya duniani WHO kuwaomba maafisa wa Chinawatoe taarifa, picha zinazowaonesha wagonjwa wakiwa wamejaa katika vyumba vya kusubiri kupatiwa huduma mjini Beijing zilionekana zikiwa zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii, pamoja na ripoti za wazazi waliokuwa wakisubiri kuwaona madaktari kwa saa nyingi au hata siku kadhaa.

Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Ghebreyesus Picha: Lian Yi/Xinhua/picture alliance

Ripoti iliyotolewa na shirika la habari linaloendeshwa na serikali ya China CCTV mapema mwezi Novemba lilitoa tahadhari kuhusu ongezeko la mlipuko wa homa ya mapafu.

Novemba 13, tume ya taifa ya afya nchini humo ilifanya mkutano na waandishi habari na kuarifu kuhusu ongezeko kubwa la "visa vya maradhi ya upumuaji hasa yanayowaathiri watoto," kulingana na taarifa ya WHO.

Jumapili, maafisa wa nchi hiyo waliagiza kufunguliwa kwa zahanati kote nchini humo ili kukabiliana na ongezeko la wagonjwa wanaohitaji kupewa tiba. Zanahati za kukabiliana na homa huanzishwa katika idara za dharura za hospitali ili kufanya vipimo kugundua maambukizi hatari, na kuzuia yasisambae ndani ya maeneo mengine ya hospitali.

Utolewaji taarifa kutoka kwa maafisa wa afya ni sehemu ya tatizo

Tahadhari kwa umma nchini China na duniani kote kuhusu ongezeko la magonjwa ya mfumo wa upumuaji zinaendelea kutolewa licha ya Shirika la Afya Duniani na maafisa wa afya wa China kusema kuwa ongezeko zaidi la visa vya homa na mafua "si jambo ambalo halitarajiwi".

Hali ya sasa imefufua kumbukumbu za China na shirika hilo kukosolewa kwa kukosa uwazi katika kuwasilisha taarifa za afya mwanzoni mwa janga la ugonjwa wa UVIKO-19 ulioanza katika mji wa Wuhan mwishoni mwa mwaka 2019.

Muonekano wa virusi vya RSV vinavyosababisha moja ya magonjwa ya upumuaji Picha: CDC via AP/picture alliance

Profesa Dong Yan Jin wa Chuo Kikuu cha Hong Kong amesema mwenendo mbaya wa utoaji taarifa kutoka kwa maafisa wa afya wa China kumechangia watu kuingiwa na hofu na kusababisha mkanganyiko miongoni mwa wazazi wenye watoto wanaougua.

Hata hivyo, kaimu mwenyekiti wa Idara ya kujiandaa na kuzuia magonjwa ya mlipuko wa WHO, Maria Van Kerkhove, aliiambia tovuti y habari za afya ya STAT katika mahojiano ya wiki iliyopita kuwa, kiwango cha maradhi ya kupumua kwa watoto huko China, ni kidogo kuliko kipindi kabla ya kuibuka kwa janga la UVIKO.

Mifumo maalumu ya China imeshawekwa tayari kufuatilia magonjwa ya homa ya mafua na maambukizi kwenye njia ya upumuaji. Pamoja na hilo, daktari mkuu katika idara ya magonjwa ya kuambukiza kwenye hospitali ya You'an ya mjini Beijing, Li Tongzeng, aliliambia gazeti la Global Times kuwa visa vipya vya magonjwa ya mfumo wa upumuaji vinaweza kuongezeka kati ya miji iliyo kaskazini mwa China.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW