1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China inaonekana kuibuka na ushindi dhidi ya janga la Corona

18 Machi 2020

Shughuli zimeanza kurudi kama kawaida nchini China, katika ishara kuwa nchi hiyo imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kudhibiti kuenea kwa virusi vya Corona licha ya kuwa kiini cha mlipuko vya virusi hivyo.

China Wuhan | Coronavirus | Xi Jinping, Präsident (picture-alliance/Photoshot)I
Rais Xi Jinping wa ChinaPicha: picture-alliance/Photoshot

Migahawa imeanza kufunguliwa huku idadi ya watu wakikusanyika tena katika mabustani, hiyo yote ikionyesha ishara kuwa China inaibuka na ushindi katika vita vyake dhidi ya virusi vya Corona ambavyo vimeutikisa ulimwengu.

Kwa wakati huu, China imeweka mikakati ya kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo kwa kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa kuvaa barakoa na pia kupima viwango vya joto mwilini kwa watu wanaoingia katika maeneo ya umma.

Pia migahawa imeweka sheria za kuwazuia watu kukaribiana wanapokula ndani ya migahawa hiyo. Mikakati yote hiyo, licha ya ugumu wake katika utekelezaji lakini inaonekana kuzaa matunda.

Sehemu kubwa ya nchi hiyo sasa imeondoa vikwazo na watu wameanza kurudi kazini, tofauti na nchi za magharibi ambapo serikali zimeanzisha marufuku ya usafiri.

Cao Wei ambaye ni naibu mkurugenzi katika hospitali ya ushirika ya Peking amesema: 

"Kwa sasa baada ya miezi mitatu kupambana na mlipuko huu, tunakaribia kufikia mwisho wake. Hata hivyo, tunasubiri angalau kwa mwezi mmoja mwengine kutathmini hali kabla ya kufanya maamuzi ya mwisho. Lakini hata mlipuko ukatokea tena kwa mara ya pili, sidhani kama utatusumbua kama vile mwanzo."

Watu wameanza kurudi kazini na biashara kufunguliwa

Mama na mwanawe wakiwa katika bustani la Botanischer, ChinaPicha: picture-alliance/dpa/Tass/A. Ivanov

Kadhalika mji wa kibiashara wa Shanghai pia umeanza kunawiri huku watu wakiendelea na biashara zao kama awali. Hata hivyo, wakaazi wa mji huo wanatakiwa kuwa na kitambulisho maalum kwenye simu zao chenye kuonyesha iwapo wako salama kuingia katika sehemu zenye watu wengi.

"Nahisi kuwa watu walioambukizwa virusi hivi hawawezi kutoka nje na kutangamana na wenzao, kwa hio sisi ambao tuko nje tuko salama", amesema Lai Jinfeng mwenye umri wa miaka 41.

Mnamo Machi 10 Rais Xi Jinping alitangaza wakati wa ziara yake katika mji wa Wuhan ambao ulikuwa kitovu cha mlipuko wa virusi vya Corona, kuwa nchi hiyo inakaribia kupata ushindi dhidi ya janga hilo la COVID-19 huku nao wachambuzi wa kiuchumi wakisema kuwa asilimia 90 ya biashara katika eneo la Hubei zimerudia hali yake ya kawaida.

 

Chanzo AFP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW