China yasaini mkataba wa kibiashara na Jumuiya ya ASEAN
28 Oktoba 2025
Jumuiya ya ushirikiano ya Kusini-Mashariki mwa Asia, ASEAN jana ilitia saini makubaliano ya uboreshaji wa biashara huria na China, ambayo yanatarajiwa kugusa sehemu katika sekta za uchumi wa kidijitali, kijani kibichi na sekta nyingine mpya.
Makubaliano hayo yalitiwa saini katika mkutano wa kilele wa Jumuiya ya ASEAN nchini Malaysia, ambao Rais Donald Trump alihudhuria siku ya Jumapili.
Jumuiya ya ASEAN iliyo na wanachama 11 ndio mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa China, huku biashara ya pande mbili ikifikia jumla ya bilioni 771 mwaka jana, kwa mujibu wa takwimu za jumuiya hiyo.
China inatafuta kuimarisha ushirikiano wake na ASEAN, eneo lenye pato jumla la dola trilioni 3.8, ili kukabiliana na ushuru mkubwa uliowekwa na utawala wa Rais Trump kote ulimwenguni.