China: Maandamano yaenea dhidi ya sera za kudhibiti UVIKO
28 Novemba 2022
Maelfu ya watu wameshuka mitaani kulalamikia masharti makali ya kuzuia kuenea kwa virusi vya uviko, chini ya sera ya serikali ya kiwango sufuri cha maambukizi ya ugonjwa huo. Maandamano sawa na hayo yalikuwa yakiendelea pia katika miji ya Beijing na Nanjing yakihusisha hasa wanafunzi wa vyuo vikuu.
Soma zaidi: WHO yaidhinisha chanjo ya Kichina ya Sinovac
Kujitokeza hadharani kupinga hatua za serikali ni tukio la nadra sana katika China inayotawaliwa na chama cha kikomunisti, lakini kulingana na mmoja wa waandamanji aliyejitambulisha kwa jina moja la Jiang, ugumu wa masharti waliyowekea umewatia ujasiri.
''Nahisi kama watu wanabebeshwa mzigo mzito, lakini sikudhani watu wengi hivi wangeshiriki, amesema Jiang na kuongeza kuwa ''hili limenibadilisha mawazo, kwa sababu nilidhani katika China ya sasa isingewezekana kuratibu kitu kama hiki.''
Jiang ameongeza kuwa ''kila mtu anajua kuwa mnamo miaka michache ya nyuma, uhuru wetu wa kujieleza kwa njia mbali mbali umebanwa kabisa. Sikuamini itafika siku tukusanyike mitaani kuelezea matakwa yetu.''
Chanzo ni jumba lililoungua moto mjini Urumqi
Kilichoanzisha maandamano haya ni hasira iliyotokana na vifo vya watu kumi waliouwa baada ya jengo lao kushikwa na moto katika mji wa Urumqi kenye jimbo la kaskazini magharibi la Xinjiang wiki iliyopita.
Soma zaidi: Ugonjwa wa Covid-19 sio kisingizio cha kuuminya uhuru wa kusema
Taarifa zilizosambaa mitandaoni zilieleza kuwa juhudi za uokozi zilikwamishwa na masharti makali ya kutotoka nje katika kuzuia kusambaa kwa virusi vya UVIKO. Zilisema huduma za wazima moto zilicheleweshwa, na baadhi ya watu waliogopa kulikimbia jengo hilo lililoungua kwa hofu ya kukiuka masharti ya vizuizi.
Maeneo mengi ya mkoa wa Xinjiang, ukiwemo mji wake mkuu, Urumqi, yamekuwa chini ya sheria hiyo kwa zaidi ya siku 100.
Sauti zapazwa kudai uhuru wa kujieleza
Katika kilichotafsiriwa kama upinzani dhidi ya kunyamazishwa, waandamanaji walibeba karatasi zisizo na maandishi yoyote, huku wakitamka maneno haya, ''ondoa amri ya kusalia majumbani,'' na ''Hatutaki kuchukuliwa vipimo, tunataka uhuru.''
Mbali na Beijing, Shanghai na Nanjing, miji ya Chengdu, Chongqing na Wuhan pia imeshuhudia maandamano makubwa.
Licha ya hatua kali za kudhibiti maambukizi ya UVIKO, hivi sasa China inakabiliwa na ongezeko la visa vya ugonjwa huo, la juu zaidi tangu kuripuka kwa janga hilo mwaka 2019. Leo hii, Tume ya Afya mjini Beijing imeripoti visa vipya 40,000.
Vyanzo: dpae, rtre