1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiAsia

China na Marekani wakaribia kuafikiana kuhusu TikTok

15 Septemba 2025

Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent amesema kumefikiwa makubaliano ya mfumo kuhusu umiliki wa jukwaa maarufu la kijamii la video la TikTok baada ya mazungumzo kati ya Marekani na China.

Indonesia Jakarta 2025 | TikTok-App na picha ya Donald Trump pamoja na bendera ya Marekani
Picha hii ni mfano wa nembo ya programu ya TikTok kama inavyoonekana kwenye simu huku Rais wa Marekani Donald Trump akiwa nyuma ya bendera ya Marekani Picha: Adriana Adie/ZUMA/picture alliance

Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent amesema kumefikiwa makubaliano ya mfumo kuhusu umiliki wa jukwaa maarufu la kijamii la video la TikTok baada ya mazungumzo ya biashara kati ya Marekani na China yaliyofanyika nchini Uhispania.

Besent alisema katika mkutano na waandishi wa habari baada ya awamu za hivi karibuni za mazungumzo ya biashara, mazungumzo kati ya mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa zaidi ulimwenguni, yaliyohitimishwa huko Madrid kwamba Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa China Xi Jinping huenda wakakamilisha makubaliano hayo kwenye mazungumzo yao ya Ijumaa.

Hatua hii imewezeshwa na Rais Trump na Xi, amesema Bessent. Lakini maafisa wa China bado hawajathibitisha taarifa hiyo ya Bessent na wala hawakuwepo kwenye mkutano huo na waandishi wa habari.

Mazungumzo ya Madrid yalifanyika katika raundi ya nne ya majadiliano ya kibiashara kati ya Marekani na China tangu Trump alipoanzisha vita vya ushuru kwenye bidhaa za China mwezi Aprili.

Kwa sasa, serikali zote mbili zinajipanga kwa ajili ya mkutano wa kilele kati ya Trump na Xi, ingawa pia bado hili halijathibitishwa. Wachambuzi wanasema kuna uwezekano mivutano ya sasa ya kibishara ikafanya mkutano huo kuchelewa kufanyika.

TikTok ni mojawapo ya programu zaidi ya 100 zilizotengenezwa katika muongo mmoja uliopita na ByteDance, kampuni ya teknolojia iliyoanzishwa mwaka 2012 na mjasiriamali wa China Zhang Yiming na yenye makao yake makuu huko kaskazini-magharibi mwa Beijing.

Mnamo 2016, ByteDance ilizindua jukwaa la video fupi linaloitwa Douyin nchini China na kisha toleo la kimataifa linaloitwa TikTok. Kisha ikanunua Musical.ly, jukwaa la kuigiza matamshi "lip-syncing" linalopendwa na vijana wa Marekani na Ulaya, na kuliunganisha na TikTok huku ikiendelea kuiweka programu hiyo tofauti na Douyin."

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW