China na Marekani zatupiana maneno makali juu ya COVID-19
25 Septemba 2020Siku mbili baada ya rais Donald Trump kutumia hotuba yake ya kila mwaka katika mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa kuishambulia China, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa pia alizungumza kwa hasira, hali iliyozua maneno makali kutoka kwa mwenzake wa China.
"Lazima niseme imetosha! mmesababisha shida kubwa kwa ulimwengu", alisema mwanadiplomasia wa China katika Umoja wa Mataifa Zhang Jun, alipoueleza mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliofanyika kwa njia ya vidio na kuhudhuriwa na wakuu wa mataifa kadha.
"China inapinga na kukataa madai yasiyo na msingi kutoka kwa Marekani. Kwa muda mrefu baadhi ya wanasiasa wa Marekani wamekuwa wakishambulia nchi nyingine na taasisi za Umoja wa Mataifa, wakitumia vibaya majukwaa yake na barala la Usalama, Marekani imekuwa ikieneza virusi vya kisiasa na kutoa habari za uongo, kutengeneza mivutano na migawanyiko".
Maneno ya mwanadiplomasia huyo yalikuja baada ya balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Kelly Craft, awali kutoa kauli zilizowakasirisha wenzao wa China. Craft alisema kwamba amechukizwa na wajumbe wa baraza la usalama ambao wametumia fursa hiyo kuzingatia chuki za kisiasa badala ya suala kuu lililopo kwa hivi sasa.
"Mnajua! ni aibu kwa kila mmoja wenu. Nimeshangazwa na kuchukizwa na yaliyokuwemo kwenye majadiliano ya leo. Kwaweli ninasikia aibu na baraza hili. wajumbe wa baraza ambao wametumia fursa hii kuzingatia chuki za kisiasa badala ya suala muhimu tulilonalo"
Kwa upande wake katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kwamba ulimwengu umeshindwa kushirikiana katika kuukabili ugonjwa wa COVID19. Guterres ameongeza kuwa ikiwa ulimwengu utashughulikia changamoto za majanga kwa utengano, hali itakuwa mbaya zaidi. "Kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa ni matokeo ya kukosekana kwa utayari, ushirikiano, umoja na mshikamano".
Mbali na wanadiplomasia hao wa China Marekani kutupiana maneno makali, viongozi mbalimbali wa Afrika walitumia mkutano huo kutoa wito wa usaidizi zaidi wa kimataifa, wakihofu kuwa janga la ugonjwa wa COVID-19 linaweza kuathiri maendeleo.
Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangangwa yeye aliomba msaada kwa Umoja wa Mataifa katika kuviondoa vikwazo vya nchi za Magharibi akisema vinarudisha nyuma malengo ya maendeleo. "Kuna ukiukaji wa sheria za kimataifa na zinaathiri uwezo wa Zimbabwe wa kutekeleza na kufikia malengo ya maendeleo endelevu. Kwa hiyo tunatoa wito kwa mkutano mkuu kukataa vikali vikwazo hivi haramu vya upande mmoja".
Naye rais mpya wa Burundi Evariste Ndayishimiye akionekana katika hadhara ya ulimwengu kwa mara ya kwanza alisema kuwa Burundi "imeweka misingi kwa ajili ya demokrasia" hata kama upinzani na makundi ya haki za binadamu yanaonya kuwa kuna mabadiliko kidogo kutoka kwa mtangulizi wake. Makundi ya haki za binadamu yanadai kuwa vitisho bado vingalipo Burundi na Ndayishimiye amewateua maafisa ambao wako chini ya vikwazo vya kimataifa kwa ukiukaji wa haki za binadamu.