1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMyanmar

China na Myanmar zasaka amani kufuatia ghasia za mpakani

Sylvia Mwehozi
31 Oktoba 2023

Waziri wa usalama wa umma wa China amefanya mazungumzo na uongozi wa kijeshi wa Myanmar juu ya upatikanaji wa amani katika mpaka wa nchi hizo mbili, kufuatia ghasia baina ya makundi ya wapiganaji na jeshi la Myanmar.

Myanmar Namhsan | Kundi la waasi la TNLA
Wapiganaji wa kundi la waasi la Ta'ang National Liberation Army (TNLA) wakishika doria karibu na mji wa Namhsan katika Jimbo la Shan kaskazini mwa Myanmar.Picha: AFP

Maelfu ya watu wameripotiwa kukimbia mapigano, huku baadhi yao wakivuka mpaka na kuingia China, baada ya makundi matatu ya wapiganaji walio na silaha wanaopiginia uhuru kuanzisha mashambulizi ya pamoja dhidi ya utawala wa kijeshi, ambao umedai kwamba umepoteza udhibiti wa baadhi ya vituo.

Waziri wa usalama wa umma wa China Wang Xiaohong ambaye pia ni mwanachama wa baraza la mawaziri  likijulikana pia kama Baraza la kitaifa la China, amekutana na kufanya mazungumzo na waziri wa mambo ya ndani wa Myanmar Luteni Jenerali Yar Pyae katika mji mkuu wa Myanmar wa Naypyidaw. Maafisa hao wamejadili suala la "amani na utulivu katika maeneo ya mpaka wa nchi hizo mbili" pamoja na ushirikiano wa kiusalama.

Majeneza yakiwa yamepangwa karibu na makaburi wakati mazishi ya watu wengi yakifanyika baada ya shambulio la kijeshi kwenye kambi ya watu waliokimbia makazi yao karibu na mji wa Laiza kaskazini mwa Myanmar.Picha: AFP

Tangu Ijumaa iliyopita, mapigano yamehanikiza katika jimbo la kaskazini mwa Myanmar la Shan, ambako mradi wa mabilioni wa reli ulio sehemu ya mradi mkubwa wa ujenzi wa miundombinu na barabara wa Beijing unaojulikana kama BELT umepangwa kuanzishwa.

Soma pia: Utawala wa kijeshi wa Myanamar na serikali ya Urusi wasaini mkataba wa ushirikiano kuhusu shughuli za uchaguzi

Makundi matatu ya wapiganaji ya Myamanr yalitangaza kuvishikilia vituo kadhaa vya kijeshi sambamba na barabara muhimu zinaiunganisha nchi hiyo na China ambayo ni mshirika wake mkubwa wa kibiashara.

Makundi hayo matatu ambayo wachambuzi wanasema yana uwezo wa kuwa na wapiganaji takribani 15,000 yamekuwa yakipigana mara kwa mara na jeshi juu ya uhuru na udhibiti wa rasilimali.

Umoja wa Mataifa umekadiria kwamba kiasi cha watu zaidi ya 6,000 wameyakimbia makaazi yao kutokana na mapigano hayo, ikiwemo 600 waliokimbia kupitia mpaka wa China.

Elimu kwa Warohingya bado kitendawili

03:09

This browser does not support the video element.

Bonyeza hapa: Warohingya wakumbuka miaka sita ya mauaji ya halaiki

Beijing imekuwa ni mshirika mkuu na msambazaji mkubwa wa silaha kwa watawala wa kijeshi wa Myanmar na imekataa kutaja unyakuzi wa madaraka wa 2021 kuwa ni mapinduzi.

Wakati huohuo maafisa wa Myanmar wamewasili hii leo nchini Bangladesh kukutana na wakimbizi wa Rohingya kama sehemu ya mpango wa muda mrefu wa kuwarejesha nyumbani unaoungwa mkono na China. Bangladesh inawahifadhi wakimbizi takribani milioni moja wa Rohingya, wengi wao walikimbia ukandamizaji wa jeshi la Myanmar mnamo mwaka 2017, suala ambalo kwa hivi sasa liko chini ya uchunguzi wa mauaji ya kimbari ya Umoja wa Mataifa.

Wakimbizi hao wa Rohingya wasio na utaifa na wanaoteswa wamekuwa wakiishi katika kambi zenye msongamano, hatarishi na zenye rasilimali kidogo huku juhudi kadhaa za kufikia makubaliano ya kuwarejesha nyumbani zikishindwa kutokana na kusitasita kwa Myanmar na wakimbizi wenyewe.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW