China na Ujerumani zakaribiana zaidi katika biashara
24 Mei 2018Mbali na kukubaliana katika baadhi ya mengi ya masuala muhimu ya usalama duniani, Merkel na viongozi hao wa China wameahidi kuimarisha ushirikiano katika masuala kama biashara na teknolojia. Rais Xi Jinping amesema ushirikiano kati ya China na Ujerumani ni mapana na ya kina kuliko wakati wowote mwingine, hapo kabla."
Merkel pia alitoa wito wa kuimarisha mahusiano , akisema kwamba nchi hizo mbili "haziwezi kukaa na kubweteka hivi sasa , licha ya kila kitu ambacho kimepatikana." amesisitiza umuhimu wa kuyafikia masoko na ushirikiano na mataifa mengine. Katika mkutano wa hapo kabla na waandishi habari , pamoja na waziri mkuu wa China Li Keqiang , Merkel alisema makubaliano na Iran sio mazuri sana, lakini mbadala una shaka zaidi.
Hali ya baadaye ya makubaliano na Iran , yenye lengo la kupunguza kasi ya hatua za Iran kuelekea kupata silaha za kinyuklia, yameingia mashakani baada ya Marekani mapema mwezi huu kuamua kujitoa kutoka katika makubaliano hayo yaliyotiwa saini na mataifa yenye nguvu duniani na kurejesha vikwazo dhidi ya nchi hiyo.
Makampuni ya Ulaya kukimbia Iran
Vikwazo huenda vikayafukuza makampuni ya Ulaya kutofanya biashara nchini Iran , hali itakayoacha nafasi kwa mataifa mengine kuingia, Merkel alisema , akidokeza kuhusu uwezo wa China kujihusisha zaidi na Iran.
"Kufuta makubaliano hayo kunahatarisha amani na uthabiti katika eneo hilo," Li amsema. Viongozi hao wawili pia wametoa wito kwa rais wa Marekani Donald Trump na kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un kuendelea na majadiliano kwa ajili ya kuondoa kabisa silaha za kinyuklia katika Korea kaskazini.
Trump na wawakilishi kutoka Korea kaskazini wamesema wanaweza kuvunja mazungumzo hayo ya kihistoria kati ya Marekani na Korea kaskazini, yanayopangwa kufanyika mwezi Juni.
Merkel alisema ameona "mambo yenye kuleta matumaini sana hivi karibuni" kuhusiana na uondoaji wa silaha za kinyuklia katika rasi ya Korea.
Kuhusiana na biashara, Li aliyaahidi makampuni ya Ujerumani kwamba sekta ya fedha na huduma nchini China itafungua milango zaidi.
Usawa wa masoko
"Hatutaacha kufungua milango," alisema katika mkutano na wafanyabiashara wa Ujerumani na China. Merkel alitoa wito wa kuweza kuingia kwa usawa katika masoko ya nchi hizo mbili na mfumo wa ushirikiano ukiwa na viwango sawa "
"Tunaweza kuona kwamba katika sekta ya magari, ushirikiano kati ya Ujerumani na China ni wa karibu sana, kuna mengi yanafanyika na ndio sababu tunataka kufanyakazi kupata mkataba wa maelewano MOU ambao utajumuisha maendeleo ya teknolojia mpya , kama magari yanayokwenda bila dereva."
"Suala la kupata fursa ya kuingia katika soko na kufanya hivyo kwa upande mwingine litachukua jukumu kubwa " katika mahusiano kati ya China na Ujerumani , Merkel alisema.
Biashara kati ya China na Ujerumani imefikia euro bilioni 190 mwaka jana. Lakini wachunguzi wanasema biashara kati ya mataifa hayo na hali ya wasi wasi imekuwa ikiongezeka katika miezi ya hivi karibuni.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Yusuf, Saumu