1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China na utamaduni wa kughushi na madawa bandia.

Sekione Kitojo31 Mei 2007

China imethibitisha kuwapo kwake makini kuhusiana na hofu iliyotanda kimataifa juu ya tabia ya kughushi na utengenezaji wa bidhaa bandia katika uchumi wake unaokua kwa kasi kwa njia inayoonekana wazi, kwa kumhukumu adhabu ya kifo mkuu wa zamani wa idara inayoweka kanuni kuhusiana na madawa nchini humo.

Zheng Xiaoyu, mkurugenzi wa zamani wa idara ya taifa ya udhibiti wa chakula na madawa, alihukumiwa kwa kupokea hongo na kushindwa kuzuwia biashara hatari na haramu ya madawa bandia. Mahakama ya mjini Beijing ilimhukumu adhabu ya kifo siku ya Jumanne asubuhi.

Adhabu hiyo kubwa inakuja baada ya wiki kadha za hofu kubwa juu ya ubora na usalama wa bidhaa za kilimo na viwanda vya madawa nchini China. China , ambayo inajipatia zaidi ya dola bilioni 30 kwa mwaka kutokana na mauzo ya nje ya chakula na madawa katika mataifa ya Asia, Marekani ya kaskazini , Ulaya na Afrika, imeshambuliwa hivi karibuni na malalamiko kutoka kila kona ya dunia kwa madai ya bidha hafifu na za hatari.

Ripoti zimeeleza kuhusu baadhi ya bidhaa ambazo zimeingizwa kemikali ambazo hazikuidhinishwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu, kamba wadogo ambao wamehifadhiwa na dawa ambayo inaweza kusababisha ugonjwa wa saratani , pamoja na uyoga ambao umepatikana na dawa za kuulia wadudu ambazo zimepigwa marufuku.

Mlolongo wa kashfa kuhusiana na mauazo ya nje ya vyakula kutoka China yamezuka baada ya kugundulika kuwa maelfu ya wanyama wafugwao majumbani nchini Marekani na Canada wamekufa baada ya kula vyakula vilivyokuwa na kemikali za sumu.

Dawa ambayo hutumika katika mbolea , ilipatikana katika ngano iliyosafirishwa kutoka China kwa ajili ya kutengenezea vyakula vya mifugo.

Sambamba na kashfa hiyo ambayo imetangazwa sana ya vyakula vya wanyama kuwa na madawa ya sumu, ilipatikana ripoti pia ya kuwa China inasafirisha nje viambato vya kutengenezea madawa ambavyo ni vya kuiga. Kiasi cha vifo 100 nchini Panama vimehusishwa na dawa ya kikohozi iliyochanganyika na dawa ya kiwandani ambayo ni ya hatari, diethylene glycol, ambayo ilitambulika kuwa ilitumiwa na kiwanda kimoja ambacho hakina leseni mashariki ya China.

Wakati malalamiko ya jumuiya ya kimataifa kuhusiana na mauzo ya nje ya China ambayo ni ya bidhaa bandia yanaendelea walaji nchini humo wamekumbana na matatizo sugu yanayohusiana na chakula na madawa kwa miaka kadha.

Zheng Xiaoyu ni afisa wa ngazi ya juu kuhusishwa na kuadhibiwa katika juhudi za China za kupambana na kurekebisha hali ya wasi wasi kuhusiana na utamaduni uliokithiri wa bidhaa bandia katika uchumi wa nchi hiyo.

Hukumu ya kifo ni sawa imesema mahakama hiyo, kutokana na hongo kubwa iliyohusika na pia athari kubwa iliyoipata nchi hiyo kutokana na Zheng kutowajibika sawa sawa.