1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China, Urusi na Cuba zapata viti Baraza la Haki za Binadamu

14 Oktoba 2020

China, Urusi na Cuba zimeshinda viti kwenye Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa jana, licha ya upinzani kutoka kwa makundi ya wanaharakati kuhusiana na rekodi mbaya za mataifa hayo kuhusu haki za binadamu.

Schweiz, Genf:  UN Human Rights Council
Picha: Reuters/D. Balibouse

Urusi na Cuba zilikuwa zinawania bila upinzani, lakini China na Saudi Arabia zilikuwa katika kinyang'anyiro cha mataifa matano kwenye mchuano pekee wa kuwania nafasi kwenye Baraza la Haki za Binadamu. Katika mchakato wa kura ya siri ndani ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 193, Pakistan ilipata kura 169, Uzbekistan 164, Nepal 159, China kura 139 na Saudi Arabia ilipata kura 90. Mwaka 2016, Saudi Arabia ilishinda kiti kwa kupata kura 152.

Licha ya mipango ya mageuzi iliyotangazwa na Saudi Arabia, shirika la haki za binadamu la Human Rights na mengine yalipinga ugombea wa Saudi Arabia, yakisema taifa hilo la Mashariki ya Kati linaendelea kuwalenga watetezi wa haki za binadamu, wapinzani na wanaharakati wa haki za wanawake, na limeonesha uwajibikaji mdogo kwa ukiukaji wa zamani, ikiwemo mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi katika ubalozi mdogo wa saudi Arabia mjini Istanbul, nchini Uturuki miaka miwili iliyopita.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pia lilizichagua Cote d'Ivoire, Gabon, Malawi, Bolivia, Ufaransa na Uingereza kwenye baraza la haki za binadamu lenye wanachama 47. Senegal, Ukraine na Mexico zilichaguliwa pia kwa muhula wa pili wa miaka mitatu. Wanachama wa baraza hilo hawawezi kuhudumu kwa zaidi ya mihula miwili mtawalia.

Mwanamfalme wa Saudia Mohammed bin SalmanPicha: picture-alliance/AP Photo/C. Owen

China, ambayo pia ilichaguliwa kwa muhula wa pili, ilishududia uungwaji wake mkono ukiporomoka kwa asilimia 20 ikilinganishwa na kura ilizopata mara ya mwisho iliposhinda kiti 2016. China pia imekosolewa vikali na jumuiya ya kimataifa kwa ukandamizaji wa haki za binadamu, hasa dhidi ya Waislamu wa jamii ya Uingur katika mkoa wa  Xinjiang, na namna ilivyoshughulikia maandamano ya kudai demokrasia katika jimbo la Hong Kong.Saudi Arabia kikaangoni juu ya rekodi yake ya haki za binadamu

Urusi ilichaguliwa tena miaka minne baada ya kuondolewa ghafla, baada ya kuhudumu muhula mmoja, iliposhindwa kwa kura mbili tu. Utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump uliitoa nchi hiyo kwenye Baraza la Haki za Binadamu mwaka 2018 katikati ya muhula wake - kuhusiana na kile ulichokiita upendeleo uliyokithiri dhidi ya Israel na kukosekana kwa mageuzi.

Chini ya sheria za Baraza la Haki za Binadamu, viti vinagawanywa kwa kanda kuhakikisha uwakilishi wa kijiografia. Mbali na kinyang'anyiro cha kanda ya Asia-Pasifiki, uchaguzi wa wanachama 15 wa baraza hilo uliamuliwa mapema kwa sababu makundi mengine yote ya kikanda yalikuwa na nafasi zisizo na ushindani.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW