1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China ya pili kwa uuzaji wa silaha duniani

27 Januari 2020

Ripoti ya taasisi ya kimataifa ya utafiti wa amani SIPRI ya mjini Stockholm imeonyesha China ni taifa la pili kwa uuzaji silaha ulimwenguni, likiwa na makampuni manne yanayoingiza mapato makubwa ya mauzo ya silaha.

Symbolbild Waffenumsätze steigen Waffen Maschinenpistolen MP5
Picha: picture alliance / dpa

Makampuni hayo manne ambayo ni pamoja na kampuni kubwa kabisa ya kutengeneza ndege ya China na shirika la serikali linalojihusisha na masuala ya anga na ulinzi, AVIC kwa pamoja yaliuza silaha zenye thamani ya dola Bilioni 54.1 mwaka 2017, hii ikiwa ni kulingana na SIPRI ikiangazia makadirio hayo mapya.

Mauzo ya silaha yaliyofanywa na AVIC yaliyofikia dola bilioni 20.1 kwa mwaka huo wa 2017, yalililipaisha shirika hilo hadi nafasi ya sita, miongoni mwa wauzaji hao wa silaha ulimwenguni. Kampuni ya Marekani ya Lockheed Martin mwaka jana ilitajwa kuwa muuzaji mkubwa kabisa wa silaha duniani, ambapo mauzo yake yalifikia thamani ya dola bilioni 43.9.

Kampuni ya NORINCO inayozalisha vifaa kama hivi inaingia kwenye orodha hiyo ya wauza silaha wakubwa dunianiPicha: picture alliance/Xinhua/L. Bin

SIPRI inalikadiria pia shirika la serikali ya China linalozalisha aina mbalimbali za bidhaa za kijeshi kama magari yenye silaha na mifumo ya kujilinda la NORINCO, lililoshika nafasi ya nane kwa uzalishaji wa silaha ulimwenguni kwa mwaka 2017, kwamba mauzo yake yalifikia dola bilioni 17.2.

Aidha, kampuni ya kutengeneza vifaa vya umeme ya CETC ya nchini China pia imetajwa katika orodha ya makampuni 20 yanayouza zaidi silaha pamoja na shirika linalozalisha magari yenye silaha la CSGC.

Watafiti wamesema walitumia taarifa walizozikusanya kutoka vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ripoti za ukaguzi na ripoti za mwaka ili kupata makadirio yao ya mauzo ya silaha yanayofanywa na makampuni ya silaha ya China. 

Watafiti hao wa SIPRI walichunguza kipindi cha kati ya mwaka 2015 hadi 2017. Mtafiti wa SIPRI wa kitengo kinachohusu mipango ya matumizi na silaha jeshini, Nan Tian ameliambia shirika la habari la DPA kwamba mbinu ya utafiti huo ilikuwa muhimu kwa sababu kimsingi kila kitu ni cha siri.

Meli ya kwanza kutenegezwa nchini China.Picha: picture-alliance/dpa/Imaginechina/W. Xizeng

Makampuni hayo manne yanachangia takriban robo ya matumizi ya jeshi la China, ambayo mwaka 2017 yalifikia kiasi dola bilioni 228, hii ikiwa ni kulingana na makadirio ya SIPRI.

China katika miaka ya karibuni imelenga kujitegemea katika uzalishaji wa silaha za teknolojia ya kisasa, ripoti hiyo imesema.

Tian amesema China hapo awali ilitegemea zaidi silaha zilizoingizwa kutoka Urusi, ambayo hivi sasa imewageukia wanunuzi wengine. Amesema hatua hiyo imekuwa miongoni mwa masuala yaliyoibua mashaka kutokana na kutokuwepo kwa uwazi na kitisho cha kusambaa zaidi kwa silaha.

Taarifa zaidi zilihitajika kuhusu makampuni mengine yaliyojikita nchini China na yanayouza silaha, ikiwa ni pamoja na makampuni makubwa mawili yanayotengeza meli. Ukubwa wa makampuni hayo umeweza pia kuwaingiza kwenye orodha ya makampuni hayo 20. Orodha hiyo inadhibitiwa na uwepo wa makampuni mengi ya Marekani.

SIPRI imesema hapo awali ilishindwa kuyahusisha makampuni hayo ya China kutokana na kutopata taarifa, lakini takwimu hizo mpya huenda zikaanza kuingizwa mwaka huu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW