1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAsia

China yaapa kuhakikisha usalama mpakani na Myanmar

Angela Mdungu
10 Novemba 2023

China imesema itahakikisha hali ya usalama na utulivu kwenye mpaka wake na Myanmar wakati kukiripotiwa kuwa karibu watu 50,000 wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mapigano kaskazini mwa Myanmar.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni ya China Wang Wenbin
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni ya China Wang WenbinPicha: Kyodo/picture alliance

Mapambano nchini Myanmar yameshika kasi katika jimbo la Shan lililo mpakani na China katika kile wachambuzi wanakiita kuwa ni changamoto kubwa tangu jeshi liliponyakua madaraka nchini Myanmar mwaka 2021.

Wizara ya mambo ya kigeni ya China kupitia msemaji wake Wang Wenbin imezitaka pande zinazohusika na mzozo nchini Myanmar kutafuta suluhu na kuwa China itatimiza majukumu yake ya kiusalama katika eneo la mpaka.

Beijing mara kadhaa imetoa miito ya kumalizika kwa vita na kuitaka Myanmar ishirikiane na China katika kuimarisha usalama na kuzuia watu kuendelea kujeruhiwa.

Soma zaidi: Kiongozi wa Myanmar asema uasi unatishia kulisambaratisha taifa

Hayo yanajiri wakati rais wa Myanmar,  inayotawaliwa na jeshi amesema kwamba nchi hiyo iko kwenye hatari ya kusambaratika kutokana na kushindwa kudhibiti machafuko katika eneo la mpaka na China. Watawala wa kijeshi wa Myanmar wanakabiliwa na changamoto kubwa tangu walipoingia madarakani kwa njia ya mapinduzi miaka miwili iliyopita.

Wanajeshi wa Myanmar wakiwa katika moja ya maeneo yenye mzozo kwenye jimbo la ShanPicha: STR/AFP/Getty Images

Changamoto hizo zinatokana na ongezeko la mashambulizi yanayofanywa na watu wanaounga mkono demokrasia pamoja na waasi kutoka makundi ya walio wachache  wanaolenga ngome za jeshi katika maeneo ya kaskazini, kaskazini mashariki, kaskazini magharibi na kusini mashariki.

China yataka usalama kwa raia wake na taasisi zake zilizopo Myanmar

Wiki iliyopita, msaidizi wa Waziri wa mambo ya kigeni wa China, Nong Rong aliitembelea Myanmar na kuitaka ichukue hatua stahiki ili kuimarisha usalama wa taasisi na wafanyakazi wa China wanaoishi nchini humo.

Katika hatua nyingine, Shirika la Umoja wa Mataifa limesema kuwa, watu 50,000 wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mapigano hayo yaliyoanzishwa na muungano wa makabila kwa kushirikiana na makundi ya wanamgambo dhidi ya jeshi kaskazini mwa Myanmar.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu shughuli za msaada wa kibinadamu OCHA imesema, huduma za simu na mtandao zilivurugika nje ya mji wa Lashio hali iliyotoa changamoto ya kutolewa kwa misaada ya kiutu kutokana na machafuko hayo.

Ofisi hiyo ya shirika la Umoja wa Mataifa  limeongeza kuwa vikwazo vya usafiri na upatikanaji wa fedha pia vilikuwa vikikwamisha juhudi za mashirika ya kiutu kutoa misaada.