1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yachukua hatua zaidi kukabiliana na virusi vya Corona

24 Januari 2020

China imechukua hatua zaidi katika kukabiliana na virusi vya Corona ambavyo vimewaua watu 25 na kusababisha zaidi ya watu 800 kuambukizwa. Kutokana na virusi hivyo usafiri wa umma umesimamishwa kwenye miji 10, kufungwa.

China Coronavirus
Picha: picture-alliance/Xinhua/X. Yijiu

Maafisa wa afya wamesema wanahofia kwamba kiwango cha maambukizi kinaweza kuongezeka kwa kasi wakati wa sherehe za mwaka mpya nchini China, ambako mamilioni ya Wachina husafiri kwenda makwao na nje ya nchi wakati wa mapumziko ya sikukuu hizo zinazoanza Ijumaa.

Kwa mujibu wa Tume ya Afya ya Taifa, hadi sasa visa 830 vya virusi vya Corona vimethibitishwa na watu 25 wamekufa, huku mamilioni wengine wakiwekwa kwenye karantini katika harakati za kudhibiti usisambae zaidi. Visa vingi vimeripotiwa katikati mwa mji wa Wuhan, ambako inaaminika virusi hivyo vilianzia katika soko ambalo linauza kimagendo nyama za wanyamapori.

Mripuko wa Corona sio dharua ya kimataifa

Jana Shirika la Afya Duniani, WHO liliutangaza mripuko wa virusi vipya vya Corona kama dharura kwa China pekee, lakini sio dharura ya kimataifa. Visa ambavyo sio vya kutisha vimeripotiwa pia nchini Thailand, Vietnam, Japan, Korea Kusini, Taiwan na Marekani na kwenye miji iliyo chini China ya Hong Kong na Macau. Hatua hiyo imesababisha mashirika ya ndege kuahirisha safari zake za ndege kuingia na kutoka Wuhan.

Eneo linakojengwa hospitali ya kuwatibu wagonjwa wa virusi vya CoronaPicha: imago images/Xinhua

Maafisa wa China wamewashauri pia watu kujizuia kwenda kwenye maeneo yenye watu wengi. Baadhi ya maeneo matakatifu ya kuabudia, ambako watu wanapeleka dhabihu wakati wa sherehe za mwaka mpya wa China yanafungwa kuanzia Ijumaa.

Wakati huo huo, China imesema inaharakisha kujenga hospitali mpya ndani ya muda wa siku 10 maalum kwa ajili ya kuwatibu wagonjwa walioathirika na virusi vya Corona. Ujenzi wa hospitali hiyo itakayokuwa na uwezo wa kuwalaza wagonjwa 100, unatarajiwa kumalizika February 3.

Katika hatua nyingine wanasayansi wamesema juhudi za kuitafuta chanjo dhidi ya virusi vya Corona, zinaweza kuchukua muda wa mwaka mmoja. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la kimataifa linaloshughulika na chanjo, GAVI Seth Berkley amesema wanasayansi hawana ufahamu wa kutosha kuhusu ugonjwa huo mpya ili kuweza kutathmini hatari yake. Hata hivyo, Berkely amesema chanjo ya kuzuia virusi vya Corona ni rahisi zaidi kutengenezwa kuliko chanjo ya malaria na virusi vya Ukimwi na itachukua miezi kadhaa kabla haijaanza kujaribiwa.

Wakati hayo yakijiri, viwanja vya ndege katika eneo la Ghuba vimesema kuwa vitaanza kuwakagua abiria wote wanaowasili kutoka China. Hatua hiyo imeenda mbali zaidi kuliko ile iliyochukuliwa na maeneo makuu ya usafirishaji barani Ulaya na Marekani, ambako wamepunguza kuwakagua abiria wanaoingia kutoka Wuhan.

(AFP, DPA, AP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW