China yaonesha nguvu kwa luteka nzito karibu na Taiwan
14 Oktoba 2024Jeshi la China lilianza awamu mpya ya mazoezi ya kijeshi karibu na Taiwan siku ya Jumatatu, ambapo lilisema kuwa ni "onyo" dhidi ya "vitendo vya kujitenga kutoka kwa wapambania uhuru wa Taiwan." Hakukuwa na tarehe yoyote iliyotolewa ya kumalizika kwa mazoezi hayo.
"Uhuru wa Taiwan na amani katika Bahari ya Taiwan haviwezekani kuungana," alisema msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Mao Ning.
Aliongeza kwamba "vichochezi kutoka wapambania uhuru vitakumbana pasina shaka na hatua za majibu."
Rais wa Taiwan, Lai Ching-te, ambaye amekuwa akizungumza waziwazi dhidi ya Beijing, ameahidi "kulinda demokrasia ya Taiwan, na kuhakikishia usalama wa kitaifa," huku Wizara yake ya Ulinzi ikisema imepeleka "vikosi vya kutosha."
Aliongeza kuwa serikali yake haihitaji kuchochea mwelekeo wa mzozo na China.
'Onyo kali'
Mazoezi hayo, yaliyopewa jina la Joint Sword-2024B, "yanapima uwezo wa pamoja wa operesheni za vikosi vya kamandi ya eneo hilo," ilisema Wizara ya Ulinzi ya China.
"Mazoezi haya pia yanatoa onyo kali kwa vitendo vya kujitenga vya wasaka uhuru wa Taiwan. Ni operesheni halali na ya lazima kwa kulinda uhuru wa taifa na umoja wa kitaifa," iliongeza.
Soma pia: China yafanya majaribio ya kombora la masafa marefu
Mazoezi haya yanafanyika katika "eneo la kaskazini, kusini na mashariki ya Kisiwa cha Taiwan," kulingana na Kapteni Li Xi, msemaji wa Kamandi ya Mashariki ya Jeshi la China.
Meli na ndege za China zinaisogelea Taiwan kwa "ukaribu kutoka maeneo tofauti," zikijikita katika doria ya maandalizi ya vita vya baharini na angani, kuzingira bandari muhimu na maeneo, kushambulia shabaha za baharini na ardhini, na "ukamataji wa pamoja," ilisema kamandi hiyo.
Baadaye Jumatatu, Wizara ya Ulinzi ya Taiwan ilisema kwamba ndege 125 na meli 17 za kivita zilihusika katika mazoezi hayo, lakini hakuna hata moja iliyovuka eneo la ulinzi la maili 24 la kisiwa hicho. Wizara ilisema inazingatia kwa makini nguvu za makombora za Beijing.
"Ndege 125 ni kiwango cha juu kabisa cha siku moja tulichokiona hadi sasa," alisema Luteni Jenerali Hsieh Jih-sheng katika mkutano wa waandishi wa habari.
Taiwan inajibu vipi?
Katika kujibu, Wizara ya Ulinzi ya Taiwan ililaani "tabia isiyo ya busara na kichochezi" kutoka bara. Wizara hiyo ilisema imepeleka "vikosi vya kufaa kujibu ipasavyo ili kulinda uhuru na demokrasia" na kutetea uhuru wa Taiwan.
Serikali ya Taiwan pia ilisema mazoezi ya hivi karibuni ya kivita ya China na kukataa kwake kuacha matumizi ya nguvu ni "vichochezi vya wazi" vinavyohatarisha amani na utulivu wa kanda.
Katika kukabiliana na vitisho zaidi vya kisiasa, kijeshi, na kiuchumi kutoka China katika siku za karibuni, Taiwan haitarudi nyuma wala kukubali, lilisema Baraza la Mambo ya Bara la Taiwan katika taarifa.
Soma pia: China yaonya juu ya vita vya Taiwan baada ya luteka za kijeshi
Taiwan pia ilisema Jumatatu kwamba ilimtia nguvuni raia mmoja wa China baada ya "kuvamia" eneo lake.
Mtu huyo aligunduliwa mapema asubuhi kwenye boti ya mpira akijaribu "kuvuka kinyume cha sheria" kuelekea kisiwa kidogo cha Menghu, kilisema Kikosi cha Ulinzi wa Pwani cha Taiwan katika taarifa.
"Si jambo lisilowezekana kwamba jaribio la mtu huyo wa kuvuka kwa boti ndogo linaweza kuwa uvamizi wa eneo la kijeshi," kilisema kikosi cha ulinzi wa Pwani.
Visiwa vya mbali vya Taiwan vimewekwa kwenye tahadhari ya juu kutokana na mazoezi ya kijeshi ya China.
Lai asema Taiwan itakabiliana na jaribio la kuinyakua
Taiwan ambayo China inaichukulia kuwa eneo lake, ilikuwa kwenye tahadhari ya mazoezi mengine ya kivita tangu hotuba ya Rais Lai Ching-te katika siku ya kitaifa iliyopita.
Katika hotuba yake, Lai aliahidi "kuzishinda juhudi za kuunganisha" kisiwa hicho, na kudai kuwa Beijing na Taipei "haziko chini ya kila mmoja."
Soma pia: Lai: China kamwe haiwezi kuiwakilisha Taiwan
Beijing iliikosoa hotuba hiyo baada ya Lai kusema China haina haki ya kuiwakilisha Taiwan, licha ya kupendekeza kushirikiana na Beijing.
China ilifanya mazoezi ya Joint Sword-2024A karibu na Taiwan kwa siku mbili mwezi Mei, mara tu baada ya Lai kuingia madarakani.
Marekani yalaani mazoezi ya China
Marekani ililaumu mazoezi ya kijeshi ya China karibu na Taiwan, ikisema kuwa hatua hiyo ni "isiyohitajika na inahatarisha uchochezi" huku ikiitakaa Beijing kuchukua hatua za kiasi.
"Marekani ina wasiwasi mkubwa kuhusu mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya Jeshi la Uokozi la Wananchi katika Bahari ya Taiwan na karibu na Taiwan," alisema msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Matthew Miller, katika taarifa, akirejelea jeshi la China.
Kupanuka huku kunakuja siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken, kuionya China dhidi ya kuchukua hatua kufuatia hotuba ya Lai wakati wa sherehe za siku ya kitaifa ya kisiwa hicho.