1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

China yaiahidi Iran uungwaji mkono thabiti

14 Februari 2023

Rais wa China Xi Jinping ametaka suala la mkataba wa kimataifa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran litatuliwe kwa haraka na kwa njia muafaka, huku akiiahidi nchi hiyo ushirikiano usioyumba.

Besuch von Irans Präsident Raisi in China
Picha: Iranian Presidency/dpa/picture alliance

Amesema hayo wakati alipomkaribisha mgeni wake, Rais Ibrahim Raisi wa Iran kwenye ikulu yake Beijing, huku akielezea uungaji mkono wa nchi yake kwa jamhuri hiyo ya Kiislamu katika kulinda haki na masilahi yake. 

Kulingana na ripoti kwenye shirika la Habari linalomilikiwa na serikali ya China CCTV, wakati wa mazungumzo kati ya rais Xi Jinping na mgeni wake Ebrahim Raisi, Jinping alimwambia Raisi kwamba nchi yake itashiriki ipasavyo kwenye mazungumzo ya kurejesha mkataba wa nyuklia kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran na utekelezaji wake.

Macron, Netanyahu wazungumzia kitisho cha Iran

Iran yasema kuwa tayari kufufua makubaliano ya nyuklia

Hiyo ni ziara ya kwanza ya kitaifa kuwahi kufanywa na rais wa Iran nchini China kwa Zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Uungwaji mkono wa China kwa Iran

Shirika la Habari la CCTV limeripoti kwamba Xi amesema China inaiunga mkono Iran kutetea uhuru wake, mipaka yake na heshima yake ya taifa, na inapinga msimamo wa upande mmoja na msimamo mkali.

Rais Xi Jinping (Kulia) akimsalimu mgeni wake rais wa Iran Ebrahim Raisi mjini Beijing, wakati Raisi akianza ziara rasmi ya siku tatu nchini humo. Februari 14, 2023.Picha: AP/picture alliance

Kiongozi huyo wa China ameongeza kuwa nchi yake inapinga hatua ya nchi za nje kuingilia masuala ya ndani ya Iran, kuhujumu usalama na utulivu wake na kwamba nchi yake itaendelea kukuza njia imara na za haraka kusuluhisha suala la nyuklia ya Iran.

"Haijalishi mabadiliko yaliyopo ya kikanda au kimataifa, China haitayumba katika kuimarisha ushirikiano rafiki na Iran,” amesema Xi.

Kabla ya kuanza ziara yake nchini China, Rais Ebrahim Raisi aliandika makala iliyochapishwa kwenye jarida linadhibitiwa na serikali yake People's Daily, iliyosema nchi Iran na China zinaamini kwamba hatua za kijumla kama vile kuweka vikwazo visivyofaa ni vyanzo vikuu vya migogoro na ukosefu wa usalama ulimwenguni.

Katika makala hiyo, Raisi aliitaja China kama rafiki wa tangu zamani na kusema juhudi za Iran kuimarisha uhusiano nayo hazitaathiriwa na hali za kikanda na kimataifa.

Marekani yaendelea kuvutana na Iran

01:08

This browser does not support the video element.

China na Iran zasaini mikataba kadhaa

Kulingana na CCTV, pande hizo mbili zimesaini makubaliano kadhaa ya ushirikiano katika sekta za kilimo, biashara, utalii, uhifadhi wa mazingira, afya, utamaduni, michezo na utoaji misaada wakati wa majanga.

China na Iran zina uhusiano imara wa kiuchumi. Mnamo mwaka 2021, nchi hizo zilisainia makubaliano ya ushirkiano wa kimkakati.

Iran, Urusi na China zafanya luteka za kijeshi kaskazini mwa bahari ya Hindi

Nchi zote mbili zinakabiliwa na shinikizo kutoka mataifa ya Magharibi kuhusu misimamo yao juu ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, mnamo wakati Iran ipo chini ya vikwazo vya Marekani kuhusiana na mpango wake wa nyuklia.

Mkwamo wa mkataba

Makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yamekuwa yakiyumbayumba tangu Marekani ilipojiondoa mwaka 2018.Picha: AEO Iran/AFP

Makubaliano ya kimataifa yaliyosainiwa mwaka 2015 kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, yaliizuia Iran kurutubisha urani, na iliiwekea Iran hali ngumu ya kutengeneza silaha za nyuklia.

Kwa upande mwingine, Iran ingenufaika kwa kuondolewa vikwazo vya kimataifa dhidi yake. Iran ilisema inatengeneza nishati ya nyuklia kwa sababu za amani.

Lakini mwaka 2018, aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump aliiondoa nchi yake kwenye mkataba huo, akisema haukuwa umefanikisha mengi kudhibiti shughuli za kinyuklia za Iran. Badala yake Trump alivirudisha vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran.

(Vyanzo: RTRE, FPAE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW