1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yaidhinisha sheria kulinda mali binafsi

P.Martin16 Machi 2007

Mkutano wa kila mwaka wa Bunge la China umemalizika leo hii katika mji mkuu Beijing. Kikao hicho cha siku 12 kimehitimishwa kwa kupitisha sheria itakayohifadhi mali za binafsi nchini humo.

Rais Hu Jintao akiingia Bunge la Watu wa China
Rais Hu Jintao akiingia Bunge la Watu wa ChinaPicha: AP

Baada ya kuwa na majadiliano makali kwa miaka mitano katika chama cha kikomunisti cha China, hatimae imepitishwa sheria ya kulinda mali za binafsi nchini humo.Sheria hiyo imeidhinishwa na asilimia 97 ya wabunge 2,889 walioshiriki katika mkutano wa siku 12 wa Baraza la Kitaifa la Umma. Afisa anaeshughulikia masuala ya kisheria bungeni,Wang Shengming amenukuliwa akisema kuwa sheria hii mpya inalinda mali za serikali na za binafsi sawa sawa na huonyesha moyo wa kufanya mageuzi na kuifungua China na wakati huo huo, inahifadhi sheria za soko la uchumi wa kijamaa. Hata hivyo,kwa maafisa wanaojulikana kama ni wafuasi wa mrengo mpya wa kushoto,katika nchi ambako mali kwa jumla hudhibitiwa na serikali, sheria hii mpya ni kama mapinduzi au ni mbegu ya mapinduzi.Wao wanauliza ni kiwango gani cha ujamaa kilichobakia katika soko la uchumi wa kijamaa.Hilo ni suala halali,wakati huu ambapo nchini China,mwanya kati ya mapato ya wamasikini na matajiri unazidi kuwa mkubwa na ambako ulajirushwa umetapakaa.

Lakini nchini China kuna sheria isiyoandikwa kwamba ilimradi chama cha kikomunisti hushughulikia utajiri unaokua,utawala wa chama kimoja usishukiwe.Lililo muhimu ni ukuaji wa kiuchumi.Na kwa sababu hiyo,serikali iliyopita, chini ya uongozi Jiang Zemin,iliwaruhusu wamiliki mali,kuingia katika chama cha kikomunisti.Hatua hiyo ilifanikiwa sana,kwani katika mwaka 2005 peke yake wamiliki mali wapatao 1,500 walijiunga katika chama cha Kikomunisti.

Lakini Rais Hu Jintao na Waziri Mkuu Wen Jiaboa wamepinga mkondo wa wastani fulani uliofuatwa na mtangulizi wao.Kwa maoni ya viongozi hao wawili,China inapaswa tena kuwa na ujamaa wake. Ukuaji wa kiuchumi uendelezwe na wakati huo huo uwepo usawa katika ugawaji wa mavuno ya juhudi hizo.Hata hivyo,viongozi hao wawili wanafahamu kuwa ni lazima kuwaridhisha hata wananchi wa tabaka ya kati.Hao ni kama watu milioni 150 waliofanikiwa kujinunulia nyumba zao wenyewe. Baadae familia hizo katika nchi inayoruhusu kuwa na mtoto mmoja tu,hutazamia kumrithisha mali, mtoto huyo pekee.Wananchi hao wana umuhimu katika kuendeleza sekta ya biashara ya kibinafsi,kwani wanachangia theluthi mbili ya pato la ndani.

Kwa upande mwingine hata haki za wakulima zinaimarishwa.Kwa mujibu wa sheria mpya iliyopitishwa,wakulima lazima walipwe fidia ya haki,wanaponyanganywa ardhi yao,ambacho ni kitisho kinachozidi kukabiliwa na wakulima nchini China.Lakini mkulima kijijini akimshtaki katibu wa chama mahakamani ana nafasi gani ya kushinda. Kupitishwa kwa sheria haimaanishi kuwa sheria hiyo inatekelezwa.Hapo ndio kuna haja ya kuwepo uhuru wa vyombo vya habari,kulaani matumizi mabaya ya mamlaka.Vile vile ungekuwepo usimamizi huru kuhakikisha kuwa sheria hiyo mpya inaheshimiwa.Lakini hadi hivi sasa,hakuna cho chote kile kilichotamkwa kuhusu mambo hayo mawili.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW