China yaionya Marekani kuhusu Korea kaskazini
15 Aprili 2017Korea ya kaskazini imeionya Marekani kuacha mhemko wake wa kijeshi ama itakabiliwa na hatua ya kujibu mashambulizi wakati kundi la meli zilizobebeba ndege za kivita zikielekea katika eneo hilo huku kukiwa na hofu kwamba Korea kaskazini huenda ikafanya jaribio lake la sita la silaha za kinyuklia.
Mamia ya magari ya kijeshi yaliyobeba watu ambao walikuwa wakiimba na kushangiria wakielekea katika gwaride la kuadhimisha mwaka wa 105 wa kuzaliwa kwa muasisi wa taifa hilo , sherehe ambazo zinaingiliana na kitisho cha hivi karibuni kabisa cha taifa hilo lenye uficho dhidi ya Marekani na rais Donald Trump.
Wasi wasi umeongezeka tangu jeshi la majini la Marekani kuishambulia Syria katika kituo cha jeshi la anga kwa makombora 59 chapa Tomahawk wiki iliyopita kujibu shambulio baya ya gesi ya sumu. Hatua hiyo imezusha maswali kuhusiana na mipango ya rais Trump kwa Korea kaskazini , ambayo imefanya majaribio ya makombora na nyuklia ikikaidi vikwazo vya Umoja wa mataifa na nchi binafsi.
Marekani itashindwa
"Hatua zozote za uchokozi zinazofanywa na Marekani katika nyanja za siasa , kiuchumi na kijeshi ikifuata sera zake za uadui kuelekea Korea kaskazini zitashindwa kwa hatua kali zitakazochukuliwa na jeshi na watu wa Korea kaskazini," shirika la habari la Korea kaskazini KCNA limesema, likinukuu msemaji wa mnadhimu mkuu wa jeshi la wananchi wa Korea.
"Hatua yetu kali ya kujibu mashambulizi dhidi ya Marekani na meli zake za kivita zitachukuliwa kwa njia ambayo hakutakuwa na huruma na bila kumpa nafasi mchokozi kunusurika."
Imesema mhemko wa "dhati wa kijeshi wa utawala wa rais Trump, umefikia katika awamu hatari amayo haiwezi kamwe kupuuziwa."
Makamu wa rais wa Marekani kwenda Korea
Marekani imeonya kwamba sera za uvumilivu wa kimkakati kuelekea Korea kaskazini zimefikia mwisho. Makamu wa rais wa Marekani Mike Pence anasafiri kwenda Korea kusini kesho Jumapili(16.04.2017) katika ziara ndefu ya siku 10 katika mataifa ya Asia.
China, mshirika pekee mkubwa wa Korea kaskazini na ambayo ni nchi jirani hata hivyo inapinga mpango wake wa silaha , jana Ijumaa kwa mara nyingine tenma imetoa wito wa mazungumzo ili kutuliza mzozo huo.
"tunazitaka pande zote kujizuwia na uchokozi na kutishiana, iwapo ni kwa maneno ama vitendo, na kutoifanya hali hiyo kuingia katika hatua ambayo haitaweza kubadilishwa na kushughulikiwa," waziri wa mambo ya kigeni wa China Wang Yi amewaambia waandishi habari mjini Beijing.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Sudi Mnette