China yaishutumu Marekani kusambaza taharuki kuhusu Corona
3 Februari 2020Wakati huo huo China imekamilisha hospitali mpya kwa ajili ya wagonjwa wa homa ya virusi vya corona mjini Muhan, wakati idadi ya vifo ikipanda na kufikia watu 360.
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni nchini China Hua Chunying amesema katika mkutano wa kila siku na waandishi habari kuwa Marekani haitatoa "msaada wowote wa maana" na imekuwa tu ikisambaza hali ya taharuki.
Marekani siku ya Ijumaa ilitangaza dharura ya kiafya na marufuku ya muda ya raia wa kigeni kuingia ambao walisafiri kwenda China katika muda wa wiki mbili zilizopita, katika hatua ya kujaribu kupambana na kusambaa kwa virusi vya corona. Vizuwizi vingine vipya vitawekwa pia kwa raia wa Marekani, ambao kurejea kwao kutoka katika jimbo kulikozuka ugonjwa huo kutasababisha wao kuwekwa katika mahali maalum ambapo watakaa huko kwa muda wa siku 14 kwa uchunguzi.
Pamoja na hayo China imekamilisha ujenzi wa hospitali kwa ajili ya wagonjwa wa virusi hivyo vya corona. Hospitali ya Huoshenshan, ikimaanisha mungu wa moto, ilijengwa katika muda wa wiki mbili , wakati maafisa wakichukua hatua za haraka kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo unaoambukizwa kupitia virusi vya corona ambapo watu 17,000 nchini humo wameambukizwa.
Hospitali yakamilika
Hospitali hiyo mpya ambayo , itakuwa na wauguzi na madaktari 1,400 na vitanda 1,000, iko tayari kupokea wagonjwa leo Jumatatu, mkurugenzi mkuu wa hospitali hiyo Zhang Siming amekieleza kituo cha utangazaji cha taifa CCTV.
China pia imesema inahitaji kwa haraka vifaa vya kitabibu vya kujikinga. Hofu ya virusi imewaingia watu katika nchi hiyo yenye idadi kubwa ya watu wanaofikia bilioni 1.4, katika vifaa vya kufunika mdomo na pua ambavyo hutumika mara moja tu, wakati waganga wanaohusika katika matibabu ya wagonjwa wa virusi hivyo katika vituo vya matibabu wameripoti upungufu wa vifaa hivyo.
"Kile ambacho China inahitaji haraka kwa sasa ni "vifuniko hivyo vya pua na mdomo,nguo maalum za kujikinga, pamoja na miwani maalum," msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Hua Chunying amesema katika taarifa kwa waandishi habari.
Wakati huo huo katika mji wa Hong Kong mamia ya wafanyakazi wa hospitali wameanza mgomo leo kudai serikali ifunge mpaka na China bara ili kuzuwia kusambaa kwa virusi vya corona na kupunguza shinikizo katika sekta ya fya.
nayo Urusi inapanga kuanza kuwaondoa raia wake kutoka mji wa Wuhan, kitovu cha ugonjwa wa virusi vya corona, na imesitisha safari za moja kwa moja za treni kwenda China.