China yajadili mipango ya amani na Ukraine
24 Julai 2024Wizara ya mambo ya nje ya China imesema viongozi hao wawili walifanya mazungumzo mjini Guangzhou, huku msemaji wake Mao Ning akiwaambia waandishi wa habari kwamba walizungumzia kuhusu mzozo wa Ukraine.
Soma pia:Kuleba yuko ziarani Beijing kutafuta amani nchini Ukraine
Ning amesema mawaziri hao wawili wa mambo ya nje walibadilishana mawazo kuhusu mzozo wa Ukraine na kwamba Wang alisema kwamba mgogoro wa Ukraine umeingia mwaka wa tatu, mzozo bado unaendelea, na kuna hatari ya kuongezeka na kuenea.
China yasema inaunga mkono juhudi zinazochangia amani
Ning ameongeza kuwa wanaunga mkono juhudi zote zinazochangia amani na wako tayari kuendelea kutekeleza jukumu muhimu la kuwezesha usitishaji mapigano na kuanza tena kwa mazungumzo ya amani.
Soma pia: Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine yupo Beijing kwa mazungumzo ya kumaliza vita
Wang amesema kuwa China inatilia maanani sana uhusiano wake na Ukraine. Akizungumzia kuimarika kwa biashara kati ya nchi hizo mbili, Wang amesema mahusiano hayo yameendelea kukua kwa hali ya kawaida licha ya ugumu na hali za kimataifa na kikanda zinazobadilika kila mara.
Ukraine pia inataka kufuata mkondo wa amani
Katika taarifa, Kuleba amesema Ukraine pia inataka kufuata mkondo wa amani na maendeleo.
Kiongozi huyo wa Ukraine ameongeza kusema ana uhakika hayo ndio masuala ya kipaombele na ya kimkakati wanayoshiriki kwa pamoja na kwamba uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umeharibu amani na kurudisha nyuma maendeleo.
Hata hivyo, Kuleba amesema Ukraine iko tayari kufanya mazungumzo na Urusi iwapo nchi hiyo iko tayari kufanya mazungumzo kwa nia safi ijapokuwa haijaona ishara yoyote kufikia sasa.
Kuleba ni afisa wa kwanza mkuu wa Ukraine kufanya ziara nchini China tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mnamo Februari mwaka 2022.
Zelensky aliishtumu China kwa kuisaidia Urusi
Ziara hiyo ya Kuleba inafuatia shutuma kuelekea China kutoka kwa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy mwezi Juni. Zelensky aliishutumu China kuisaidia Urusi kuzuia nchi kushiriki katika kongamano la amani la Uswisi. China ilikanusha madai hayo.
Urusi yasema Ukraine ilifanya shambulizi dhidi ya hospitali ya watoto
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi Maria Zakharova leo amesisitiza kuhusu msimamo wa Urusikwamba hospitali ya watoto mjini Kyiv iliyolengwa mnamo Julai 8, ililengwa na makombora ya ulinzi wa anga ya Ukraine na kukanusha shtuma za Ukraine kwamba lilikuwa shambulizi la Urusi.