1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yajaribu 'kuhujumu' mfumo wa haki wa Marekani

25 Oktoba 2022

Maafisa wakuu wa sheria nchini Marekani wameishutumu serikali ya China kwa kuendeleza kampeni isiyokoma ya kijasusi, kuhujumu mfumo wa haki wa Marekani na kuiba siri za kibiashara.

US-Justizminister Garland
Picha: Susan Walsh/AP/dpa/picture alliance

Mwanasheria mkuu wa serikali wa Marekani Merrick Garland pamoja na mkurugenzi wa shirika la upelelezi la Marekani FBI Christopher Wray, wameeleza kwa kina visa vitatu tofauti ambapo maafisa wa ujasusi wa China walituhumiwa kuwanyanyasa wakosoaji wao ndani ya Marekani. Wametaja pia kisa cha kujaribu kuhujumu kesi dhidi ya kampuni kubwa ya simu nchini China Huawei na vilevile kuwashinikiza baadhi ya wasomi wa Marekani kuwafanyia kazi.

Raia kumi na watatu wa China waliotuhumiwa kufanya kazi na mashirika ya kijasusi ya China wamefunguliwa mashtaka, na wawili wametiwa nguvuni.

Garland ameeleza kuwa kesi hizo zimeonesha kuwa China ilitaka kuingilia haki na uhuru wa watu binafsi ndani ya Marekani na kuhujumu mfumo wa mahakama unaolinda haki hizo.

"Wizara ya Sheria haitaruhusu majaribio ya nchi ya nje kuhujumu sheria, ambayo ni msingi wa demokrasia yetu," amesema mwanasheria mkuu wa Marekani.

Garland na wakuu wengine wa mahakama walizungumza na waandishi wa habari mjini Washington kuhusu kesi hizo, siku moja tu baada ya rais wa China Xi Jinping kuchaguliwa kihistoria kwa muhula wa tatu kama kiongozi wa nchi yake.

Wray: Juhudi za kijasusi za China dhidi ya Marekani zimeongezeka katika muongo uliopita

Maafisa hao wamemhusisha Rais Xi na kile walichosema kuwa juhudi ambazo zimekuwa zikiongezeka katika muongo uliopita wa mashirika ya kijasusi ya China kuiba hakimiliki za Marekani na kuwakandamiza wapinzani wa kisiasa wa China walioko Marekani.

Mkurugenzi wa FBI Christopher Wray aisema visa vya kijasusi vya China dhidi ya Marekani vimeongezeka.Picha: Chip Somodevilla/Pool/Reuters

Hata hivyo Wray hakujibu swali la ikiwa tangazo hilo lilipangwa kuwa sambamba na uthibitisho wa Chama cha Kikomunisti cha China kumchagua tena Rais Xi kuwa Katibu wake mkuu Jumapili iliyopita.

"Ikiwa serikali ya China na chama cha Kikomunisti cha China vitaendelea kuvunja sheria zetu, basi wataendelea kukumbana na FBI,” amesema Wray.

Katika kesi moja iliyotajwa jana lakini iliyozinduliwa wiki iliyopita, raia saba wa China walidaiwa kujaribu kumlazimisha mkaazi wa Marekani kurudi China. Watu wawili miongoni mwao walikamatwa, lakini wengine watano wanaoshukiwa kuwa wafanyakazi wa mashirika ya ujasusi ya China bado hawajapatikana, huku ikishukiwa huenda wamesharudi China.

Kesi dhidi ya kampuni ya Huawei

Katika kesi ya pili, majasusi wawili wanaoifanyia China kazi, walijaribu kumsajili mfanyakazi wa serikali, ili kuwapa taarifa za ndani ya mahakama kuhusu mashtaka dhidi ya kampuni ya Huawei.

Mnamo mwaka 2019, Huawei ilishtakiwa kwa tuhuma za kufanya kampeni ya kimfumo kuiba siri za biashara za Marekani, ukwepaji vikwazo miongoni mwa mashtaka mengine.

Kampuni ya Huawei inakabiliwa na kesi Marekani ya kushiriki kampeni ya kimfumo kuiba siri za biashara za Marekani.Picha: Artur Widak/NurPhoto/picture alliance

Majasusi hao wawili, waliamini kwamba wamefanikiwa kumsajili afisa huyo wa serikali na kumlipa kwa sarafu ya mtandaoni bitcoin zenye thamani ya dola 61,000, ili awape hati kuhusina na kesi dhidi ya Huawei.

Lakini kumbe afisa huyo alikuwa jasusi pia wa Marekani aliyekuwa akifanya kazi na FBI.

Kesi ya tatu iliwahusu majasusi wa China waliofanya kazi na wizara ya Usalama wa nchi huku wakijifanya kuwa wasomi, wanaowasajili majasusi nchini Marekani.

Kampeni ya kijasusi isiyokoma ya China inayolenga Marekani

Tangu mwaka 2008 hadi 2018, walilenga kuwasajili maprofesa, maafisa wa zamani wa usalama na maafisa wengine wenye taarifa nyeti, na teknolojia.

"Katika kesi hizi zote tatu, na maelfu nyingine, tulikuta kwamba serikali ya China inatishia taratibu zetu za kidemokrasia na utawala wa sheria, huku wakilenga kuhujumu usalama wa uchumi wa Marekani na haki za kimsingi za binadamu," amesema Wray.

Wizara ya Sheria ya Marekani imetangaza takriban nusu dazeni ya kesi kama hizo za madai kama hayo dhidi ya maafisa wa ujasusi wa China mwaka huu.

Wray ameongeza kuwa kitisho hicho ni cha mara kwa mara, na kwamba kila baada ya saa 12, maafisa wa FBI hufungua uchunguzi wa kijasusi dhidi ya China.

(AFPE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW