1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yamhukumu mfanyabiashara wa Canada miaka 11 jela

Sylvia Mwehozi
11 Agosti 2021

China imemhukumu kifungo cha miaka 11 jela mfanyabiashara wa Canada katika kesi ya ujasusi inayohusishwa na jitihada za Beijing za kushinikiza kuachiwa kwa mkurugenzi wa kampuni ya Huawei anayeshikiliwa nchini Canada. 

China | Kanadischer Geschäftsmann Michael Spavor | Beijing Capital International Airport
Picha: Kim Kyung-Hoon/REUTERS

Mfanyabiashara Michael Spavor na mwanadiplomasia wa zamani wa Canada Michael Kovrig walitiwa nguvuni katika kile wakosoaji wamekielezea kuwa ni "utekaji nyara wa kisiasa" baada ya mkurugenzi wa kampuni ya Huawei Meng Wanzhou kukamatwa mnamo Desemba mosi mwaka 2018 katika uwanja wa ndege wa Vancouver nchini Canada. Spavor amehukumiwa katika mahakama ya Dandong iliyoko kilometa 340 mashariki mwa Beijing kwenye mpaka wa kaskazini na Korea.

Serikali ya China inamtuhumu Spavor kusambaza taarifa nyeti kwa mwanadiplomasia wa zamani Michael Kovrig, mwanzoni mwa mwaka 2017. Wote wawili walikuwa wametengwa na hawajakuwa na mawasiliano na wanadiplomasia wa Canada. Serikali ya Canada imelaani adhabu ya Spavor ikisema yeye na mwenzake Kovrig wanashikiliwa "kinyume na sheria" na kutaka kuachiwa haraka.

Balozi wa Canada mjini Beijing Dominic Barton amedai kuwa mchakato wa kisheria katika kesi dhidi ya Spavor umekosa "haki na uwazi".

"Tunalaani kwa nguvu zote uamuzi huu uliotolewa ambao mchakato wake wa kisheria ulikosa haki na uwazi. Na tulisema tangu awali kwamba Michael Spavor na Micheal Kovrig walikamatwa kiholela na tutaendelea kushinikiza kuachiwa kwao. "

Spavor ana muda wa hadi wiki mbili wa kukata rufaa. Wanadiplomasia kutoka Marekani, Japan, Uingereza, Australia, Ujerumani na nchi nyingine za Umoja wa Ulaya walikusanyika nje ya ubalozi wa Canada mjini Beijing kwa ajili ya kuonyesha mshikamano. Pia wametoa taarifa tofauti ya kutaka Spavor na Kovrig kushitakiwa kwa haki au kuachiwa huru.

Michael Kovrig (kushoto) na Michael Spavor(kulia)

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema katika taarifa yake kwamba "kushitakiwa kwa raia wawili wa Canada ni pigo kubwa zaidi katika utawala wa China wa kuimarisha utawala wa sheria".

Meng, ambaye ni Mkurugenzi na binti wa mwanzilishi wa kampuni ya teknolojia ya Huawei alikamatwa kwa kuzingatia mashitaka ya Marekani ya uwezekano wa kufanya biashara na Iran na hivyo kukiuka vikwazo vya kibiashara. Mawakili wake wanadai kwamba kesi yake imechochewa kisiasa na kile anachotuhumiwa hakitambuliki kama kosa nchini Canada.Marekani yaipiga marufuku Huawei

Kwa upande wake China ilikosoa kukamatwa kwa mkuruguenzi huyo ikisema ni juhudi za Marekani za kuzuia ukuaji wa teknolojia yake. Huawei ambayo ni kampuni kubwa ya uzalishaji wa vifaa vya teknolojia na simu aina ya smartphone, ni kampuni ya kwanza ya kimataifa ya teknolojia ya China na ambayo imekuwa kitovu cha mvutano baina ya Marekani na China juu ya teknolojia na mfumo wa usalama wa taarifa.

Hata hivyo China inakanusha kuwepo uhusiano baina ya kesi ya mkurugenzi wa Huawei na kukamatwa kwa Spavor na Kovrig. Hukumu dhidi ya Spavor inaonekana kuwa shinikizo wakati majaji wa Canada wakisikiliza hoja za mwisho juu ya kumpeleka mkurugenzi wa Huawei nchini Marekani ili kukabiliana na mashitaka yanayohusiana na uwezekano wa kukiukwa vikwazo vya kibiashara.