1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yaongeza juhudi kupambana na Corona

Angela Mdungu
21 Januari 2020

Watu sita wamefariki nchini China kutokana na virusi vya Corona. Hayo ni kwa mujibu wa Televisheni ya Taifa ya nchi hiyo. Taarifa zaidi zinasema idadi ya walioathiriwa na virusi hivyo imefikia karibu watu 300.

Corona Virus China
Picha: picture-alliance/dpa/Center of Disease Control

Mamlaka nchini humo zimeongeza tahadhari zaidi katika kupambana na mlipuko mpya wa Virusi hivyo ambavyo huenda vikasambaa zaidi. Hofu ya kusambaa kwa virusi vya Corona imetanda zaidi baada ya mtaalamu wa serikali ya China Zhong Nanshan kuweka wazi kupitia televisheni ya Taifa kuwa virusi hivyo vinaweza kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.

Visa vya awali vya virusi hivyo vilivyoripotiwa mwishoni mwa mwezi uliopita vilikuwa vikihusishwa na soko la vyakula vinavyotokana na bahari na maambukizi yalidhaniwa yanatokana na wanyama kwenda kwa binaadamu.

Habari za kusambaa kwa virusi vya Corona zimetolewa wakati shirika la Afya duniani WHO likisema litafikiria kuutangaza mlipuko huo kuwa dharura ya kimataifa ya afya ya umma. Shirika hilo la afya duniani limeongeza kuwa visa zaidi vya ugonjwa huo huenda vikajitokeza.

Mataifa mengine yaanza kuchukua tahadhari

Mji wa Wuhan ndio unaoripotiwa kuwa na visa vingi zaidi vya ugonjwa huo kwa kuwa na wagonjwa 258. Mjini Beijing, zaidi ya watu 20 wameripotiwa kupata maambukizi. Miji mingine iliyoarifiwa kuwa na visa vya virusi hivyo ni pamoja na Shanghai na kusini mwa jimbo la Guangdong. Korea Kusini, Japan na Thailand ambako kuna wasafiri wengi kutoka China kumeripotiwa visa vinne vya ugonjwa huo.

Baadhi ya nchi zinazohofiwa kuathiriwa na virusi vya Corona

Huku kukiwa na wasiwasi wa mlipuko wa virusi hivyo kusambaa duniani kama ilivyokuwa kwa virusi vya SARS vilivyosambaa kutoka China kwa nchi kadhaa mwaka 2002-2003, baadhi ya mataifa yameanza kuchukua hatua za tahadhari kwa kuwapima wasafiri wanaotoka China hasa Wuhan. 

Wakati huohuo makampuni ya usafiri wa anga ya China yalitangaza kuwa hayatotoza ada kwa watu waliokwisha kununua tiketi watakaotaka kuahirisha safari kutokana na hofu ya mlipuko wa virusi vya Corona. Mlipuko wa virusi hivyo umetokea huku mamilioni ya watu wa bara la Asia wakijiandaa kusafiri kwa ajili ya kusherehekea mwaka mpya wa Lunar wiki hii.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW