1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yaongoza kupokea utayari wa wakimbizi duniani

Lilian Mtono19 Mei 2016

Ripoti ya Shirika la kimataifa la haki za binadamu, Amnesty International, iliyotolewa alhamisi hii, inayataja China, Ujerumani na Uingereza kuwa ni mataifa yaliyo na utayari zaidi wa kuwakaribisha wakimbizi

Picha: picture-alliance/dpa/A.Mehmet

Raia kutoka nchi za Urusi, Indonesia na Thailand wanashikilia mkia katika kielelezo hicho kinachohusiana na kuwakaribisha wakimbizi, kilichohusisha nchi 27, na kilichotumia kigezo cha uwezo wa jamii wa kuwakirimu wakimbizi.

Kielelezo hicho kiliyapanga mataifa katika alama kwa kuzingatia namna wakazi wake walivyozungumzia utayari wa kuwapokea na kuwakirimu wakimbizi kwenye makazi yao, majirani, katika miji mikubwa, miji midogo ama vijiji na kwenye nchi zao.

"Ilibainika kuwa ni mtu mmoja tu kati ya kumi duniani kote, ambaye angekuwa tayari kumpokea mkimbizi na kuishi naye kwenye makazi yake." Idadi hii inajionyesha dhahiri, amesema katibu Mkuu wa shirika la Amnesty International, Shalil Shetty. "Watu wapo tayari kuwakaribisha wakimbizi, lakini mwitikio usio wa kibinadamu wa serikali kuhusiana na janga la wakimbizi, haliendani kabisa na maoni ya watu wao," amesema Shetty.

Machafuko yaliyodumu kwa miaka mitano nchini Syria, yaliyosababisha vifo vya kiasi ya watu 270,000, yamechangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa janga hili la wakimbizi katika eneo la Mashariki ya Kati na Ulaya, kutokana na watu kuyakimbia mapigano.

utafiti huo ulihusisha watu 27,000

Mamilioni zaidi wanayakimbia makazi yao duniani kote kila mwaka kutokana na machafuko na majanga mengine. Nchini China, ambako kunachukuliwa kama nchi iliyo tayari zaidi kupokea wakimbizi, asilimia 46 ya watu wake wameonyesha kukubali kuwakaribisha wakimbizi kwenye makazi yao, wakati Uingereza ikiwa ni asilimia 29, wakati Ujerumani ikiwa ni asilimia 10.

Urusi ambayo inashikilia mkia miongoni mwa nchi zinazowakaribisha wakimbizi, asilimia 61 walisema hawatakubali kuwapa hifadhi kwenye nchi yao.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, Jumatano wiki hii alimtaka rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kufikiria upya maamuzi yake ya kufunga makambi mawili ya wakimbizi, ikiwa ni pamoja na kambi kubwa zaidi duniani, na kuwarudisha wakimbizi wa Somalia nchini mwao.

Kambi ya Dadaab inayotarajiwa kufungwa na serikali ya KenyaPicha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Kwenye mazungumzo kwa njia ya simu, Katibu mkuu huyo amemsihi rais Kenyatta kuendelea kuzingatia makubaliano yaliyoafikiwa Novemba 2013, pamoja na serikali ya Somalia na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi, UNHCR, kama msingi wa kuwarejesha wakimbizi hao wa Somalia katika hali ya usalama na kiutu.

Kenya ina kiasi ya wakimbizi 600,000, na miongoni mwao wameishi nchini humo kwa robo ya muongo mmoja.

Kufungwa kwa makambi hayo ya Dadaab na Kakuma kunafuatia tahadhari kuwa yamekuwa maeneo ya kuzalisha wapiganaji wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda lenye mahusiano na kundi la wapiganaji la Al-Shabaab, pamoja na kuwa kituo cha uhalifu na upitishwaji magendo.

Dadaab, iliyopo eneo la mpaka kati ya Kenya na Somalia, pia ni makaazi ya raia 350,000 na Kakuma iliyopo kaskazini magharibi mwa Kenya, nayo ikiwa na wakazi 180,000, na thelthi ya wakazi hao ni wasomali.

Tangu kuanza utekelezwaji wa makubaliano hayo ya mwaka 2013 ya kuwarejesha wakimbizi nchini Somalia, ni wachache tu waliokubali kurejea kwa hiyari yao.

Hatua hiyo ya utekelezaji kwenda taratibu kumeifanya serikali ya Kenya mapema mwezi huu kutangaza kutoendelea kupokea wakimbizi, na kwamba itayafunga mara moja makambi makuu ya wakimbizi nchini humo.

Mwandishi: Lilian Mtono/afp

Mhariri: Josephat Charo