1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

China yapinga vikali vikwazo vya Marekani

Hawa Bihoga
26 Agosti 2024

China imeelezea kutoridhika kabisaa na kupinga vikali vikwazo vipya vilivyotangazwa na Marekani dhidi ya kampuni za China, kuhusiana na uhusiano na vita vya Urusi nchini Ukraine.

Bendera ya china ikipepea kando ya Bahari.
Bendera ya china ikipepea kando ya Bahari.Picha: Daniel Berehulak/Getty Images

Tamko la China limetolewa leo na wizara ya biashara na kusema China inaihimiza Marekani kuacha mara moja vitendo vyake visivyosahihi, na kwmaba itachukuwa hatua zinazostahili kulinda haki zake halali na maslahi ya kampuni za Kichina. 

Ijumaa Marekani iliweka vikwazo vikubwa dhidi ya watu na makampuni 400 nchini Urusi na kote Ulaya, Asia na Mashariki ya Kati, ikiyashutumu kutoa bidhaa na huduma zinazowezesha juhudi za vita vya Urusi na kusaidia uwezo wake wa kukwepa vikwazo. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema ina wasiwasi na  usafirishaji wa biadhaa za "matumizi ya mara mbili" kutoka China kwenda Urusi.

Soma pia:Yellen: Marekani haitakubali viwanda kuharibiwa na China

Wizara ya Biashara nchini China katika taarifa yake ilipinga vikali Marekani kuweka makampuni mengi ya Kichina kwenye orodha yake ya udhibiti wa mauzo ya nje. Hatua hiyo inazuia kampuni kama hizo kufanya biashara na Marekani bila kupata leseni maalum ambayo kupatikana kwake ni tabu.

Wizara hiyo ilisema hatua ya Marekani ilikuwa "vikwazo vya kawaida vya upande mmoja," ikisema vitavuruga uagizaji na sheria za biashara ya kimataifa, na pia kuathiri uthabiti wa minyororo ya kimataifa ya viwanda na ugavi.

Rais wa Marekani Joe Biden akisikiliza wakati Rais China Xi Jinping akizungumza wakati wa mkutano wao, uliofanyika California, mwaka 2023.Picha: Doug Mills/AP Photo/picture alliance

"China inaitaka Marekani kuacha mara moja mazoea yake mabaya na itachukua hatua muhimu ili kulinda kwa uthabiti haki na maslahi halali ya makampuni ya China," ilisema.

Hatua hiyo ya Marekani ni ya hivi karibuni zaidi katika mfululizo wa maelfu ya vikwazo ambavyo vimewekewa makampuni ya Urusi na wasambazaji wake katika mataifa mengine tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari 2022.

Ufanisi wa vikwazo watiliwa shaka

Ufanisi wa vikwazo hivyo umetiliwa shaka hasa kwa vile Urusi imeendelea kusaidia uchumi wake kwa kuuza mafuta na gesi kwenye masoko ya kimataifa.

Kulingana na  wizara ya mambo ya nje ya Marekani, baadhi ya makampuni yenye makao yake nchini China yalitoa zana za mashine na vipuri kwa makampuni ya Urusi.

Soma pia: Urusi ilifeli kiinterejensia kuhusu uvamizi wa Ukraine Kursk?

China imejaribu kujitanabahisha kama nchi isiyoegemea upande wowote katika mzozo wa Ukraine, lakini inashiriki uhasama mkubwa wa Urusi dhidi ya mataifa ya Magharibi.

Baada ya nchi za Magharibi kuweka vikwazo vizito kwa mafuta ya Urusi kujibu Urusi kutuma wanajeshi wake nchini Ukraine mnamo Februari 2022, China iliongeza vikali ununuzi wake wa mafuta ya Urusi, na kuongeza ushawishi wake nchini Urusi.

Rais wa Urusi Vladimir Putin pia alisisitiza umuhimu wa China kwa kukutana mjini Beijing na kiongozi wa China Xi Jinping mara baada ya kuapishwa kwa muhula wa tano katika Kremlin.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW