China yaripoti maambukizi mapya 46 ya virusi vya corona
26 Julai 2020
Miongoni mwa maabukizi hayo mapya, 22 yalikuwa katika jimbo la magharibi ya mbali la Xinjiang, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na tume ya taifa ya afya.
China iliripoti kesi mbili mpya za watu walioonesha dalili, ikiwa ni chini kutoka watu 74 siku moja kabla.
Hadi Jumamosi, China bara ilikuwa na kesi za maambukizi ya virusi vya corona 83,830 zilizothibitishwa, mamlaka hiyo ya afya imesema. Vifo kutokana na COVID-19 vimefikia jumla ya watu 4,634.
Marekani siku ya Jumamosi (25.07.2020) ilirekodi maambukizi mapya ya watu 68,212 katika masaa 24 yaliyopita, chuo kikuu cha Johns Hopkins kiliripoti katika hesabu zake za kila siku. Hii inafikisha jumla ya idadi ya kesi za maambukizi katika taifa hilo lililoathirika zaidi duniani kufikia 4,174,437, chuo hicho kikuu mjini Baltimore kimesema leo Jumapili (26.07.2020).
Vifo vingine 1,067 viliripotiwa , na kufikisha idadi ya vifo katika nchi hiyo kuwa 146,391. Baada ya kupungua katika viwango vya maambukizi mwishoni mwa robo ya kwanza ya mwaka huu, Marekani imeshuhudia ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona, hususan katika majimbo ya kusini na magharibi mwa nchi hiyo kama Califonia, Texas, Alabama na florida.
Katika siku 12 zilizopita, idadi ya maambukizi mapya yanayoripotiwa kila siku imepita 60,000. Wanasayansi wanakubaliana kuwa ongezeko katika viwango vya vifo linafuatia ongezeko la maambukizi kwa wiki tatu hadi nne. Idadi jumla ya vifo kila siku kwa siku nne zilizopita imepindukia 1,000.
Korea kaskazini
Wakati huo huo Maafisa nchini Korea kaskazini wameweka vizuwizi vya kuwataka watu wasalie majumbani mwao katika mji wa mpakani wa Kaesong baada ya kugundua kile walichokiita kesi ya kwanza ya mshukiwa wa virusi vya corona, vyombo vya habari vya serikali vimeripoti leo Jumapili,(26.07.2020).
Kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong Un aliitisha kikao cha dharura cha kamati ya uongozi jana jumamosi (25.07.2020) kutekeleza "utaratibu wa dharura wa kiwango cha juu na kutoa tahadhari ya kiwango cha juu" kudhibiti virusi, shirika rasmi la habari nchini humo KCNA lilisema.
Iwapo itathibitishwa , itakuwa ni kesi ya kwanza inayotambuliwa rasmi ya COVID-19 katika taifa hilo la Korea kaskazini ambako miundo mbinu ya hospitali inaonekena kuwa na mapungufu makubwa kupambana na janga hilo.
KCNA imesema mtu mmoja aliyeikimbia nchi hiyo ambaye aliondoka na kwenda Korea kusini miaka mitatu iliyopita alirejea Julai 19 baada ya "kuvuka na kuingia nchini humo kinyume na sheria" katika mpaka wenye ulinzi mkali unaogawanya nchi hizo mbili.Lakini hakuna ripoti upande wa kusini wa mtu yeyote aliyeondoka kupitia kile ambacho ni mpaka wenye ulinzi mkali kabisa duniani, uliowekwa mabomu ya kutegwa ardhini na vituo vya ulinzi.