1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yataka mdahalo na Korea Kaskazini

24 Mei 2017

China imesema hakuna sababu ya kukataa kufanya mdahalo na Korea Kaskazini licha ya msururu wa majaribio ya makombora yaliyokosolewa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Chinesischer Botschafter bei den Vereinten Nationen Liu Jieyi
Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa, Liu JieyiPicha: Picture alliance/AP Photo/S. Wenig

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana jana katika kikao cha faragha kujadili njia za kuimarisha vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini kufuatia jaribio la kombora la masafa ya wastani Jumapili iliyopita ambalo kwa mara nyingine limeibua wasiwasi kuhusu uwezo wa kijeshi wa nchi hiyo.

China, mshirika pekee wa kibiashara wa Korea Kaskazini, imeweka bayana kwamba kufanya mazungumzo ya kidiplomasia badala ya kuweka vikwazo, ni jambo linalotakiwa kupewa kupaumbele. "Hakuna sababu kwa nini mdahalo haufanyiki katika hali ya sasa," amesema balozi wa China katika Umoja wa Mataifa Liu Jieyi alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kikao hicho.

Katika hatua inayoonekana kuwa pigo kwa Marekani balozi Liu amesisitiza kwamba wakati wa juhudi za nyuma kupunguza wasiwasi katika eneo la Korea, kila ufanisi ulipatikana kwa njia ya mdahalo.

Katika mkutano wa baraza la usalama wanachama walipewa taarifa na mkuu wa masuala ya siasa wa Umoja wa Mataifa, Jeffrey Feltman, kuhusu masuala ya kiufundi ya jaribio la Jumapili. Balozi wa Uruguay katika Umoja wa Mataifa, ambaya ni rais wa sasa wa baraza la usalama, Elbio Rosseli, amesema jaribio hilo ni la 11 tangu mwaka huu ulipoanza na inaonyesha azma ya Korea Kaskazini kumiliki silaza za nyuklia, jambo linaloibua wasiwasi mkubwa.

Kombora aina ya Pukguksong-2 lililofanyiwa majaribio Jumapili (22.05.2017)Picha: Reuters/KCNA

Jumatatu jioni baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lililanii jaribio la kombora la Korea Kaskazini na kuapa kuchukua hatua za kuimarisha vikwazo.

Korea Kaskazini yasema ina haki

Lakini mwanadiplomasia wa Korea Kaskazini Ju Yong Chol ameuambia mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuziangamiza silaha za nyuklia kwamba majaribio ya makombora ya hivi karibuni ni kitendo cha haki ya kujilinda kilichofanywa na taifa linalomiliki silaha za nyuklia na si kinyume cha sheria ya kimataifa. Chol aidha amepinga taarifa za baraza la usalama la Umoja wa Mataifa zilizotilia shaka haki ya kimsingi ya Korea Kaskazini.

"Korea Kaskazini ni taifa lenye nyuklia, mtu alitambue au asilitambue. Ingawa Marekani inajaribu kwa kila njia zote kuweka mazingira ya kimataifa ya vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini, inapasa watambue shinikizo zaidi litaipa msukumo Korea Kaskazini kuimarisha silaha zake za nyuklia na kuisukuma iandae majaribio mengine."

Chol pia amesema ni sera ya kikatili ya Marekani na luteka zake za kijeshi, vitisho vya nyuklia na kuongeza wanajeshi katika rasi ya Korea yanaoifanya hali kuwa mbaya katika eneo zima la Korea, jambo ambalo linaifanya Korea Kaskazini kuimarisha mpango wake wa nyuklia.

Akijibu kauli hiyo balozi wa Marekani anayehusika na masuala ya kuangazima silaha za nyuklia, Robert Wood, amesema Marekani si kitisho kwa Korea Kaskazini. "Kitisho kikubwa kwa utawala wa Korea Kaskazini ni utawala wenyewe na unahitaji kuheshimu majukumu yake ya kimataifa sasa. Iko chini ya vikwazo na itabaki kuwa chini ya vikwazo. Na hii kauli kwamba maazimio ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa si sheria ya kimataifa ni ujinga. Huu ni utawala unaohubiri amani lakini ni kitisho kikubwa kwa uthabiti katika eneo la Asia na Pasifiki."

Marekani imesema iko tayari kushiriki mazungumzo na Korea Kaskazini kwa masharti kwamba isitishe majaribio yake ya makombora na silaha za nyuklia. Mara kwa mara China imetaka mazungumzo ya pande sita yaliyokwama wakati Korea Kaskazini ilipojiondoa kwenye meza ya mazungumzo mwaka 2009 yaanze tena. Mbali na China na Korea Kaskazini mazungumzo hayo yanazijumuisha Marekani, Korea Kusini, Urusi na Japan.

Mwandishi:Josephat Charo/afpe/rtre

Mhariri:Iddi Sessanga