1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

China yatangaza kupungua kwa idadi ya watu wake

17 Januari 2023

China yatangaza kupungua kwa idadi ya watu wake kwa mara ya kwanza baada ya miongo kadhaa, huku taifa hilo linaloongoza kwa kuwa na watu wengi duniani likishuhudia kuongezeka kwa wazee na kupungua kwa watoto wanaozaliwa.

China | Bevölkerungswachstum
Picha: Mark Schiefelbein/AP Photo/picture alliance

Taasisi ya takwimu nchini China imesema kufikia mwisho wa mwaka 2022, taifa hilo lenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani lilikuwa na wakazi bilioni 1,41I. Hii inamaanisha watu 850,000 wamepungua ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Taasisi hiyo imeendelea kusema kuwa idadi hiyo inajumuisha tu idadi ya watu wa China Bara, ukiondoa Hong Kong na Macao pamoja na wakaazi wa kigeni. Takwimu hiyo inasema kuna watoto milioni 9.56 waliozaliwa na idadi ya vifo ya watu milioni 10.41.

Ni mara ya kwanza kwa idadi hiyo kupungua tangu kampeini ya Great Leap Forward

Hii ni mara ya kwanza kwa idadi hiyo kupungua tangu mwaka 1961, kufuatia kushindwa kwa kampeni ya uanzishaji viwanda mwishoni mwa miaka ya 1950 inayojulikana kama Great Leap Forward. Taasisi hiyo ya takwimu ya China imesema idadi ya watu waliofikisha umri wa kufanya kazi wa kati ya miaka ya 16 na 59 ilifikia watu milioni 875.56, hii ikiwa asilimia 62 ya idadi jumla ya watu nchini humo huku wale wenye umri wa miaka 65 na zaidi ikifikia watu milioni 209.78, sawa na asilimia 14.9 ya idadi jumla ya watu nchini humo.Takwimu hiyo pia zilionyesha kuongezeka kwa ukuaji wa miji katika nchi ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa ya vijiji. Katika mwaka wa 2022 idadi ya watu mijini iliongezeka kwa kiwango cha milioni 6.46 hadi kufikia milioni 920.71, sawa na asilimia 65.22, huku idadi ya wakazi wa vijijini ikipungua kwa milioni 7.31.

Idadi ya wazee yaongezeka nchini ChinaPicha: AP

Sera za zamani zilizingatia takwimu potovu

Yi Fuxian, mwanademografia na mtaalam wa mtindo wa idadi ya watu wa China katika chuo kikuu cha Wisconsin-Madison, amesema idadi ya watu wa China ilianza kupungua miaka 9-10 mapema kuliko ilivyobashiriwa na maafisa wa China na kukadiriwa na Umoja wa Mataifa. Yi ameliambia shirika la habari la Associated press kwamba hii inamaanisha kuwa mgogoro wa takwimu halisi ya idadi ya watu nchini China ni mkubwa zaidi na kwamba sera zote za zamani za kiuchumi, kijamii, ulinzi na kigeni za China zilizingatia takwimu potovu za idadi jumla ya watu nchini humo.

China yakabiliwa na kupungua kwa viwango vya watoto wanaozaliwa na kuzeeka haraka kwa watu wa jamii yake.

Mnamo mwaka 2021, idadi ya wakazi nchini humo iliongezeka kwa watu 450,000. China kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na kupungua kwa viwango vya uzazi na kuzeeka haraka kwa watu wa jamii yake.

Wanaume waliwazidi wanawake kwa idadi ya milioni 722.06 hadi milioni 689.69, matokeo ya sera kali ya mtoto mmoja ambayo ilimalizika rasmi mwaka 2016 na upendeleo wa kitamaduni wa mtoto wa kiume kuendeleza jina la familia. Mabadiliko hayo ya sera yaliobadilisha sheria ya mwaka 1979 ambayo iliweka kikomo cha mtoto mmoja kwa familia hata hivyo yalishuhudia kuongezeka kwa kiwango kidogo cha uzazi na baadaye kupungua tena. Wataalamu wengi wanasema kwamba karibu miongo minne ya sera ya mtotommoja, imebadilisha mtazamo wa kijamii nchini humo. Sasa watu wengi wamezowea kuwa na familia ndogo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW