China yaijibu Marekani vita vya kibiashara
4 Aprili 2018Wizara ya biashara pamoja na wizara ya fedha ya China zimesema orodha ya China ya nyongeza ya asilimia 25 ya ushuru kwa bidhaa za Marekani inajumuisha bidhaa 106 zenye thamani ya kibiashara ya dola bilioni 50. Tarehe ya kuanza kutekelezwa agizo hilo itategemea ni lini Marekani itakapoanza kutekeleza mpango wake.
Tangazo la China linakuja saa chache baada ya Marekani kuchapisha orodha ya bidhaa za China za thamani ya dola bilioni 50 ambazo huenda zikatozwa ushuru. Orodha hiyo ya Marekani inayojumuisha bidhaa 1,300 itadurusiwa upya katika kipindi cha siku 60 zijazo kabla uamuzi wa mwisho kupitishwa, kuamua ni bidhaa zipi zitakazotozwa ushuru zaidi wa asilimia 25.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa China, Lu Kang, ameyaeleza mapendekezo hayo ya Marekani kuwa yasiyo na msingi na ni utaratibu wa kuyalinda masoko ya ndani.
"Hatua ya Marekani inapuuzilia mbali bila kujali, manufaa yanayotokana na muundo wa ushirikiano wa kibiashara kati ya Marekani na China ambao umekuwepo kwa miongo minne iliyopita. Inapuuza miito ya jumuiya ya wafanyabiashara na masilahi ya watumiaji bidhaa katika nchi hizi mbili. Haina masilahi yoyote kwa uchumi wa China wala Marekani, na hata uchumi wa dunia."
Lu Kiang aidha amesema China itaishitaki Marekani kwa Shirika la Biashara Duniani, WTO.
Hatua ya China haikutarajiwa haraka
Wataalamu wanasema ushuru wa China kwa bidhaa za kilimo za Marekani kama maharage ya soya utawaathiri wakulima wanaotokea majimbo yaliyompigia kura rais Donald Trump. Kampuni ya kutengeneza ndege nchini Marekani, Boeing, huenda ikaathiriwa kwani shirika la ndege la China Airlines linaweza kuamua kununua ndege zaidi kutoka kwa kampuni ya kutengeneza ndege barani Ulaya, Airbus.
Tangazo hilo la China limesababisha mauzo makubwa ya hisa katika masoko ya kimataifa ya hisa na bidhaa, huku masoko ya hisa nchini Marekani yakiporomoka kwa asilimia 1.5, na hisa za maharage ya soya zikishuka thamani kwa asilimia 3.7 na thamani ya dola ikishuka mapema leo. Sarafu ya China yuan pia imeyumba.
Hatua ya China imekuja baada ya ahadi iliyotolewa na utawala wa mjini Beijing kwamba ungechukua hatua kama hizo ha kulipiza kisasi, lakini imechukuliwa haraka mno kuliko ilivyotarajiwa na wachambuzi wengi, hivyo kuongeza hofu katika masoko kwamba mataifa mawili makubwa kiuchumi ulimwenguni yanaelekea kutumbukia katiak vita vikubwa vya kibiashara ambavyo yumkini vikauyumbisha uchumi wa dunia.
Tofauti na orodha ya Marekani iliyoujumuisha bidhaa za viwanda, orodha ya China imezilenga bidhaa muhimu za Marekani zinazouzwa katika nchi za nje.
Wizara ya mambo ya nje ya China imesema imeonyesha uaminifu na uwazi katika kutaka kuusuluhisha mzozo wa kibiasahara kupitia mazungumzo, lakini fursa nzuri za kuutatua kupitia mdahalo zimepuuzwa mara kwa amara na Marekani.
Mwandishi:Josephat Charo/afpe/rtre/ape
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman