1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yatawala siku ya pili ya mkutano wa G7

5 Mei 2021

Kundi la mataifa saba tajiri duniani – G7 limejadili namna ya kuwa na msimamo wa pamoja kuelekea China inayozidi kuwa na ushawishi kote duniani katika mkutano wa kwanza ya ana kwa ana ya mawaziri wa mambo ya kigeni.

G7-Gipfel in London
Picha: Stefan Rousseau/AP Photo/picture alliance

Huku ikiunga mkono miito ya Rais wa Marekani Joe Biden ya kuwepo ushirikiano wa kina wa mataifa, nchi mwenyeji wa mkutano huo Uingereza iliwaalika wageni wakiwemo India, Korea Kusini na Australia kwa sehemu ya mazungumzo hayo yaliyoandaliwa katikati mwa London kwa siku tatu.

Mkutano wa jana ulihusu zaidi China, ambayo uwezo wake wake wa kijeshi na kiuchumi na utayari wa kutekeleza ushawishi wake vimezidi kuyatisha mataifa ya Magharibi.

Soma zaidi: Mataifa ya G7 yaungana kujadili vitisho vya ulimwengu 

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marakeni Antony Blinken ambaye pia jana alikutana na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alisema sio kusudi lao kujaribu kuidhibiti China au kuishikilia chini bali wanajaribu kuunga mkono utaratibu unaoheshimu sheria za kimataifa ambao nchi zao zimewekeza pakubwa kwa miongo mingi ya manufaa, sio tu kwa ajili ya raia wao wenyewe bali pia watu kote ulimwenguni, ikiwemo China.

Afisa mmoja mwandamizi wa Marekani amesema baada ya kikao cha jana kuwa hakukuwa na "kutokubaliana kwa namna yoyote” ndani ya G7 kuhusu China au masuala mengine.

Mkutano wa kwanza wa ana kwa ana katika miaka miwiliPicha: Ben Stansall/AP/picture alliance

Mawaziri hao wote walielezea wasiwasi kuhusu rekodi ya haki za binaadamu ya China, wakati kukiwa na hasira kuhusu kuzuiliwa makambini kwa Waislamu wa jamii ya Waighur, pamoja na sera za kulazimisha za kiuchumi za China kuelekea mataifa mengine.

Halmashauri Kuu ya Ulaya jana imesitisha juhudi za kuidhinisha mkataba mnono wa Umoja wa Ulaya wa uwekezaji na China, habari ambazo bila shaka zimekaribishwa na Marekani, ijapokuwa maafisa wamesema suala hilo halikujitokeza katika majadiliano ya G7.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Uingereza Dominic Raab ametoa wito wa kuhakikisha China inatimiza ahadi ilizotoa, ikiwemo kuhusu Hong Kong, ambayo iliahidiwa mfumo tofauti kabla ya Uingereza kukabidhi koloni hilo mwaka wa 1997.

Soma pia: G7 wataka wanajeshi wa Eritrea kuondoka Tigray

Lakini sambamba na serikali ya Biden, ambayo imebadilisha sauti na pia dhana ya msimamo mkali wa aliyekuwa rais Donald Trump dhidi ya China, Raab amehimiza kupatikana kwa mbinu za kufanya kazi na China katika njia ya busara na chanya pale ambapo inawezekana – likiwemo suala la mabadiliko ya tabia nchi.

Mmoja wa watangulizi wa Blinken kama waziri wa mambo ya kigeni, Hilllary Clinton, alisema mataifa yanahitaji kuweka shinikizo kubwa China katika kile kinachofahamika kama mahakama ya maoni ya umma.

Mawaziri hao wa mambo ya kigeni wa G7pia walijadili mgogoro unaoendelea kushuhudiwa Myanmar pamoja na hali nchini Syria, Libya na wasiwasi unaotokana na vitendo vya uchokozi vya Urusi.

Blinken leo anaelekea Ukraine kuonyesha uungaji mkono baada ya Urusi mwezi uliopita kuwapeleka wanajeshi wake 100,000 na kisha kuwaondoa kwenye maeneo ya mpaka na Crimea.

Kundi hilo la nchi 7 linajiandaa kwa mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi mwezi ujao mjini Cornwall, kusini magharibi mwa Uingereza, katika kile kitakuwa ziara ya kwanza ya kigeni ya Biden akiwa rais.

AFP

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW