1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

China yatishia hatua kali iwapo Taiwan itataka uhuru

Daniel Gakuba
29 Desemba 2021

China imeonya kuwa itachukuwa hatua kali ikiwa Taiwan itapiga hatua kuelekea kujitangazia uhuru wake. Huko Hong Kong, polisi wameifunga tovuti ya News Stand ya wanaharakati wa demokrasia.

China JH-7A Bomber
China inashikilia kuwa itaungana na Taiwan, hata kwa matumizi ya nguvu za kijeshi ikibidiPicha: Yang Pan/Xinhua/picture alliance

 

Msemaji huyo, Ma Xiaoguang, akizungumza na vyombo vya habari amesema China inao utashi wa kuungana tena na Taiwan kwa njia ya amani, na kuongeza kuwa ikiwa Taiwan itauvuka mstari mwekundu kuhusu suala la uhuru, China itachukua hatua.

Soma zaidi: Taiwan lazima iwe tayari kujilinda

''Tunatoa onyo kali kwa mamlaka ya chama cha DPP kwamba kutafuta uhuru wa Taiwan ni mbio za sakafuni zitakazoishia ukingoni,'' amesema Ma na kuongeza kuwa juhudi za kuigawa China kwa kushirikiana na wakala wa nje, vile vile kusimama katika upande unaopinga taifa la China hazitafanikiwa, na itabidi kuzizuia muda ungalipo.

Rais wa China, Tsai Ing-wen ambaye uongozi wake umeongeza mvutano na BeijingPicha: Annabelle Chih/SOPA Images via ZUMA Wire/picture alliance

Ma amesema wazalendo wa China, iwe China bara au kisiwani Taiwan wanapaswa kufanya kazi pamoja katika mipango ya amani na maendeleo, ambayo amesema itachangia katika alichokiita, 'njia ya kihistoria kuelekea enzi mpya ya ukuu wa China'.

Kigingi katika uhusiano na Marekani

China inayoongozwa na chama cha Kikomunisti hukichukulia kisiwa cha Taiwan kinachoongozwa kidemokrasia kuwa ni sehemu ya himaya yake, na mnamo miaka miwili iliyopita imeongeza shinikizo la kijeshi na la kidiplomasia kuyapa nguvu madai yake hayo, hali ambayo imeikasirisha Taiwan na kuzidisha wasiwasi nchini Marekani.

Soma zaidi: Biden aapa kuilinda Taiwan endapo China itaivamia 

Mvutano huo baina ya China na Taiwan umekuwa mwiba katika uhusiano kati ya Marekani na China, Marekani ikiwa muungaji mkono muhimu zaidi wa Taiwan kimataifa licha ya kuwa hazina uhusiano rasmi kidiplomasia.

Ingawa Marekani haina uhusiano wa kidiplomasia na Taiwan, maafisa wake wamekuwa wakikitembelea kisiwa hicho kuonyesha mshikamanoPicha: Taiwan Presidential Office/AP Photo/picture alliance

Kidiplomasia Marekani inaitambua China moja, lakini kisheria inalo jukumu la kuisaidia Taiwan kwa kuipa uwezo wa kujilinda. Ama kuhusu iwapo Washington itaingilia kati kijeshi iwapo China itashambulia, hilo ni suala linaloachwa kugubikwa na utata.

Pigo jingine kwa wanaharakati Hong Kong

Huku hayo yakiarifiwa upande wa Taiwan, tovuti ya wanaharakati wa demokrasia mjini Hong Kong imetangaza kuwa itasitisha shughuli zake, baada ya polisi kukamata wafanyakazi wake sita, wakiwemo wa sasa na wa zamani, kwa kutuhuma za kuchapisha maudhui yanayohamasisha uasi na kujitenga.

Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa mhariri mkuu wa tovuti hiyo ya News Stand, Patrick Lam ni miongoni mwa waliokamatwa, na kwamba ameonekana akiswagwa na polisi akiwa na pingu mikononi.

Soma zaidi: Rais wa China Xi Jin Ping ataka muungano na Taiwan

Shirika hilo pia limearifu kuwa maafisa wa polisi walionekana wakitoka katika ofisi za tovuti hiyo, wakibeba visanduku na vifurushi.

Polisi ya Hong Kong imethibitisha kuwa imefanya upekuzi katika ofisi za tovuti hiyo, kwa kushirikisha maafisa wapatao 200.

 

rtre, afpe

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW