1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yatishia kutoa ripoti yake juu ya haki za binadamu nchini Marekani

1 Machi 2005

China yaghadhabishwa na ripoti juu ya haki za binadamu iliyotolewa na Marekani

Ripoti ya kila mwaka juu ya haki za binadamu ya Marekani,iliyotolewa jumatatu iliishutumu vikali china kwa kukandamiza upinzani , haki za kidini na kupinga haki ya uhuru wa kuzungumza huku ripoti hiyo pia ikisema kwamba kumekuwepo na mauji ya kiholela yasiyochukuliwa hatua pamoja na mateso kwa wafungwa .

Upande wake China imeonekana kukasirishwa sana na ripoti ya Marekani na imetishia kutoa ripoti yake ya sita kuhusu haki za banadamu nchini Marekani.

Shirika la habari nchini China Xinhua limesema kwamba ripoti hiyo ya China yenye misingi ya kweli itafichua rekodi mbaya za Marekani kuhusu uvamizi wake katika mataifa mengine na jinsi inavyowatesa wafungwa ambao sio raia wa Marekani .

Ripoti hiyo pia itaandika juu ya mtazamo wa maisha,Uhuru na usalama wa kibinafsi wa raia wa Marekani,ikiwa ni pamoja na haki zao za kisiasa,Uhuru, Uchumi, haki za kijamii pamoja na haki za utamaduni,ubaguzi wa rangi, hali ya wanawake pamoja na watoto.

Msemaji katika wizara ya mambo ya nje wa China Liu Jianchao pia aliilaani ripoti ya Marekani kwa kuibua masuala ya haki za Taiwan na kusema kuwa China haitajishughulisha katika kuimarisha uhusiano wake na nchi hiyo.

Hata hivyo bwana Liu aliongeza kusema kwamba Kulindwa kwa haki za binadamu nchini China kunatekelezwa kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo na kwamba kufikia sasa serikali ya China inashughulikia suala la kuimarisha hali ya haki za binadamu katika nyanja zote ili kuikuza jamii katika umoja na amani.

Ripoti ya Marekani imekuja siku chache baada ya ripoti ya Umoja wa Mataifa kuitolea wito China kulinda haki za kikatiba na kuikosoa kwa kuwafunga jela watu wenye kutoa sauti za maoni yao ya kidini na kisiasa.

Upande wake Umoja wa Ulaya umeitaka China kuimarisha rekodi yake juu ya haki za Binadamu kabla ya kuondosha vikwazo vya silaha dhidi yake vilivyowekwa miaka 15 iliyopita jambo ambalo linapingwa naMarekani kwa kuhofia kwamba silaha hizo huenda China ikazitumia dhidi ya Taiwan.

Ripoti ya Marekani kuhusu rekodi juu ya haki za binadamu katika mataifa ya Asia kama vile Pakistan,Bangladesh,Nepal na China imebakia kuwa mbaya katika kipindi cha mwaka jana huku ikiripoti kuongezeka kwa visa vya utumiaji nguvu dhidi ya waliowachache, polisi kutumia nguvu,utumiaji mbaya wa mamlaka,pamoja na ukandamizaji wa demokrasia.

Ikigusia haki za binadamu na kisiasa nchini Pakistan ripoti imetaja hali kuwa mbaya mno hasa katika suala la haki ya uandishi ikisema imepingwa na kuwepo kwa ubaguzi wa hali ya juu dhidi ya dini za waliowachache.

Pia imegusia kwamba rais Parvez Musharraf aliyechaguliwa kupitia kura ya maoni iliyokuwa na utatanishi amebakia kuwa mkuu wa majeshi licha ya kuahidi kujiuzulu wadhifa huo mwishoni mwa mwaka jana.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW