China yaunga mkono hatua za UN kuhusu vita vya Gaza
22 Machi 2024China imesema leo kuwa inaunga mkono hatua zinazochukuliwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kumaliza vita katika ukanda wa Gaza.
Hata hivyo nchi hiyo ambayo ni mwanachama wa kudumu wa baraza hilo yenye nguvu ya kura ya turufu, haikusema iwapo itaunga mkono rasimu ya azimio la Marekani kuhusu haja ya kumaliza vita hivyo mara moja.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China Lin Jian ameongeza kuwa "China inaliunga mkono Baraza la Usalama katika kuchukuwa hatua zaidi za uwajibikaji na sahihi haraka iwezekanvyo ili kuongeza juhudi za kumaliza vita Gaza mapema, kusaidia katika janga la kibinadamu na kushinikiza kuhusu kutekelezwa kwa suluhisho la mataifa mawili."
Lin ameongeza kuwa jamii ya kimataifa inalitarajia baraza hilo kutimiza majukumu yake kikamilifu na kwamba kuhusu suala la Palestinian na Israel, lazima kuwe na heshima katika historia, ukweli na msimamo na maoni ya mataifa mengi ya Kiarabu.