1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

China yarusha makombora katika luteka karibu na Taiwan

Daniel Gakuba
4 Agosti 2022

Wizara ya Ulinzi ya Taiwan imesema China imerusha makombora ya masafa marefu katika eneo la bahari linaloizunguka Taiwan na kulaani luteka kubwa za kijeshi zinazofanywa na China ikizielezea kama kitisho kwa usalama wake.

China Säbelrasseln nach Pelosi Besuch
Meli na ndege za kivita vya China katika eneo la bahari kati ya nchi hiyo na TaiwanPicha: Hector Retamal/AFP/Getty Images

Kulingana na taarifa ya wizara ya ulinzi ya Taiwan, China imevurumusha mfululizo wa makombora aina ya Dongfeng katika maeneo ya bahari kaskazini mashariki na kusini mashariki mwa kisiwa cha Taiwan kuanzia saa nane majira ya ukanda huo.

Hata hivyo taarifa hiyo haikueleza bayana mahali yalipoanguka makombora hayo, na wala haikueleza ikiwa yalirushwa juu ya kisiwa hicho.

Soma zaidi: Pelosi asema Marekani haitaitelekeza Taiwan

Kutokana na hali hiyo, Taiwan imefuta safari zote za ndege kuingia na kutoka katika kisiwa hicho chenye mamlaka ya ndani.

Jeshi la China pia limethibitisha kuwa limeyafyatua makombora hayo. Msemaji wa kamandi ya mashariki ya jeshi hilo, Kanali Shi Yi, amesema makombora yote yamepatia shabaha, na kupima uwezo wake wa kukwepa vizuizi.

Ziara ya Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, Nancy Pelosi kisiwani Taiwan imeighadhabisha ChinaPicha: ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Ziara ya Pelosi kama kichocheo cha mvutano

Mara ya mwisho kwa China kufyatua makombora katika eneo la bahari la Taiwan ilikuwa mwaka 1996, na mara hii luteka hizi zimechochewa na ziara ya Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi kisiwani Taiwan, ambayo China imesema ni uchokozi na uingiliaji katika mambo yake ya ndani.

Soma zaidi: Biden na Xi Jinping wakabiliana kwa simu

China hukichukulia kisiwa cha Taiwan kama eneo lake lililoasi, ikiapa kulirejesha, hata kwa njia za kijeshi ikibidi.

Msemaji wa baraza la mawaziri la Taiwan amelaani vikali hatua hizo za China, akisema zinaonyesha kutowajibika na zinakiuka sheria na kanuni za Umoja wa Mataifa.

Luteka hizi za kijeshi za China kuizunguka Taiwan zinatarajiwa kudumu kwa siku nne.

Nchi za Ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Asia zimehimiza stahamala ili mzozo huu usigeuke kuwa kitisho cha kikandaPicha: Takahiro Suzuki/ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Udukuzi wa kimtandao ni silaha nyingine ya kivita

Mbali na Luteka za kijeshi kwenye bahari, msemaji huyo amesema kuwa mitandao ya ofisi ya rais, wizara ya ulinzi na ya mambo ya nje ya Taiwan imehujumiwa na wadukuzi.

Chanzo kimoja kutoka Taiwan kimeliarifu shirika la habari la Reuters kuwa kwa kipindi kifupi meli na ndege za kivita za China zilivuka mpaka wa baharini kati yake na Taiwan, na katika muda huo zana za kijeshi za pande hizo mbili zilikabiliana zikiwa karibu katika eneo moja.

Soma zaidi: China yaishutumu Marekani kwa kuipaka tope

Pande mbalimbali zimetoa kauli kuhusu yanayojiri baina ya China na Taiwan: Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Ukanda wa Asia Kusini na Mashariki, ASEAN ambao wanakutana nchini Cambodia, wamezitaka pande zote kuwa makini na kuepuka mienendo inayoweza kulizamisha eneo hilo katika mzozo.

Marekani na washirika wake katika kundi la nchi saba za kidemokrasia zinazoongoza kiviwanda, G7, wameionya China kutoitumia ziara ya Nancy Pelosi kama kisingizio cha kuivamia kijeshi Taiwan.

Vyanzo: ape, rtre

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW