China yawajia juu wanaoikosoa sheria ya usalama ya Hong Kong
20 Machi 2024Hong Kong, iliyowahi kuwa koloni la Uingereza kabla ya kukabidhiwa kwa China mwaka 1997, mapema Jumanne ilipitisha sheria hiyo ya usalama wa taifa inayokusudia kutoa adhabu kali kwa vitendo mbalimbali ambavyo mamlaka itaamua kuwa ni tishio kwa usalama wa taifa.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China Li Jian amezungumza na waandishi wa habari Jumatano na kusisitiza kauli ya serikali ya kuyakemea mataifa yaliyoikosoa sheria hiyo mpya ya usalama wa taifa ya Hong Kong na kusema kuwa serikali ya China, imeazimia kwa uthabiti kulinda mamlaka ya taifa, usalama na maslahi ya kimaendeleo, kutekeleza sera ya nchi moja yenye mifumo miwili, na kupinga uingiliaji wowote wa masuala ya ndani ya Hong Kong. Ameonya kuwa, mashambulizi yote na kuchafuliwa kwa muswada wa sheria yatashindwa na kamwe hayatofanikiwa.
Soma zaidi: Wabunge Hong-Kong wapitisha sheria mpya ya usalama
Msemaji huyo wa wizara ya mambo ya kigeni ya China ameongeza kuwa usalama ni sharti muhimu katika kuleta maendeleo, na kwamba utawala wa sheria ni msingi wa ustawi. Kulingana na kiongozi wa Hong Kong John Lee, sheria hiyo mpya iliyopitishwa inatoa adhabu kwa makosa ya uhaini, uasi, wizi wa siri za serikali na ujasusi, hujuma, na uingiliaji wa mambo ya ndani kutoka nje.
Mchakato wa sheria mpya ya usalama wa taifa ulifuata sheria
Serikali imesema kuwa mchakato wa uundwaji wa sheria hiyo ulifuata katiba ambayo imekuwa ikiiongoza Hong Kong tangu ilipokabidhiwa kwa China kutoka kwa Uingereza.
Soma zaidi: Amnesty: Sheria ya usalama wa kitaifa imeangamiza uhuru Hong Kong
Baada ya kupitishwa kwa sheria hiyo ya usalama wa taifa ya Hong Kong, Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza David Cameron alisema kuwa mchakato wa kuipitisha sheria hiyo uliharakishwa na kwamba sheria hiyo itaendelea zaidi kuharibu haki na uhuru uliopo katika mji huo.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Australia Penny Wong alimtahadharisha mwenzake wa china aliye ziarani Canberra kuwa, sheria hiyo mpya itaendelea kukiuka haki na uhuru na kuwa athari zake zitaonekana hadi nje ya China.Marekani, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, na Japan nazo pia zimepinga sheria hiyo hadharani.