China yazindua hatua mpya kuimarisha biashara ya nje
21 Novemba 2024China imetangaza hatua mpya zinazolenga kuimarisha biashara ya kigeni, huku Beijing ikipambana kuboresha uchumi wake unaozidi kutishiwa na sera zinazotarajiwa kuwa za uhasama za Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump.
Uchumi huo wa pili kwa ukubwa duniani umekuwa ukipambana kufufuka tangu mlipuko wa janga la UVIKO-19, na unaendelea kuathiriwa na na mzozo wa madeni katika sekta muhimu ya nyumba, viwango duni vya ununuzi na ukosefu mkubwa wa ajira kwa vijana. Rais Xi aongeza juhudi za kuinadi China kama kinara wa utandawazi
Hali imezidi kuwa ya mashaka kufuatia kuchaguliwa tena kwa Trump, ambaye katika muhula wake wa kwanza alipandisha pakubwa ushuru kwa bidhaa za China na kusababisha vita vya kibiashara.
Wizara ya Biashara ya China imetoa agizo kwa ngazi zote za serikali kutekeleza haraka sera tisa za kukuza biashara ya kigeni, ikiwemo kupanua bima ya mikopo ya mauzo ya nje, msaada wa kifedha kwa kampuni za kigeni, na kuboresha utatuzi wa masuala ya biashara ya mipakani.
Hatua nyingine ni kukuza biashara ya mtandao ya kuvuka mipaka, kusukuma mauzo ya bidhaa maalum za kilimo na kutoa msaada kwa uagizaji wa vifaa muhimu na nishati.