Chipukizi katika Bayern munich
17 Septemba 2007Ingawa katika msimu huu wa champions League-kombe la klabu bingwa barani ulaya unoanza kesho jumatano,mabingwa mara kadhaa wa Ujerumani-Bayern Munich hawashirki,kwavile wameangukia mara hii katika kombe la ulaya la UEFA,wameanza msimu mpya kwa kishindo ingawa walimudu sare ya bao 1:1 jumamosi walipocheza na Schalke 04.Bayern Munich wameweka rekodi katika kuchukua ubingwa wa Ujerumani.Lakini kama wasemavyo ,ukitaka kujua nguvu za timu yeyote ile angalia chipukizi wake .Kwahivyo,Bayern Munich ina shule yake binafsi ya kuwalea na kuwanoa chipukizi na inatumia kila mwaka milioni ya fedha kuigharimia.
Katika jumba la vijana la Bayern Munich,liliopo Säbenerstr. Mjini Munich,wanaishi na kujifunza dimba chipukizi wa Bayern Munich ambao keshokutwa wanatazamiwa kujiunga na klabu ya mastadi wakubwa wa dimba.Umri wao ni kati ya miaka 15 na 17.
“Haya hapa ni masanduku ya barua ya vijana 12 wanaoishi katika jumba hili la vijana wetu.Wanatoka klabu kama Eintracht Frankfurt,Darmstadt 98,klabu ya Ansbach ,Munich 1860,FC Metz,SSV Ulm,Giessen,Pfullendorf,Toni Kroos kutoka Rostock,Ganghofer kutoka Rosenheim……”
Pale Werner Kern,anapoyapotia masanduku ya barua katika jumba la chipukizi la Bayern munich,humdhihirikia haraka kwanini katika mtaa wa Säbener Str.Nr.53 mjini Munich ,mastadi wachanga wananolewa kucheza dimba.
Kern ndie kiongozi wa idara inayowahusu chipukizi katika klabu ya FC bayern Munich tangu 1998.
Tangu mwaka huo ,Kern amekuwa akitoa mastadi wa kabumbu mfululizo.Asema,
“Imefahamika nchini Ujerumani kwamba mafunzo ni jambo linalohitajika.Hadi karibuni hivi, watu walisahau jambo hilo.Mtu aliamini kwamba mastadi wa dimba wanaota katika miti.Zamani ilikua hivyo.Akina Overath,Beckenbauer au Gerd Müller-hawa bila walimu wa kuwafunza na mipango ya kuwaendeleza waliweza kutamba,kwa sababu wakicheza mpira kila siku mitaani.
Leo hii mafunzo yamebadilika.Ndio kuna dimba la mitaani, lakini sio kama ilivyokua zamasni.Mafanikio yetu ya karibuni yalioletwa na timu yetu ya Taifa ya chipukizi,yamethibitisha huu ndio mkondo barabara wa kufuata.”
Asema Werner Kern.
Msingi unaosimamia kuwachagua mastadi chipukizi ni mfumo wa scouting-mfumo wa kuwasaka na kuwachunguza chipukizi wenye ustadi wa dimba .
Lakini, katika umri huo mchanga,mpira usiwe ndio kila kitu,la hasha.Vijana 12 waliomo kwenye mtandao kati ya umri wa miaka 15 na 17 kutoka klabu ya Toni Kroos, walichaguliwa wachezaji bora kabisa wa kombe la dunia chini ya umri wa miaka 17,sio tu wanajipatia mafunzo bora ya dimba kwa gharama ya Bayern Munich,bali wanaishi na wanakula katika jumba hilo la vijana la klabu hiyo.
Isitoshe wanajipatia mafunzo ya shule ya kawaida na sio kucheza mpira tu.
Mwalimu wao ni Florian Cichler nae anasema:
“Wanafunzi hawa wa dimba hawapotezewi wakati wao wa masomo na Bayern Munich.”
Anaongeza kusema wanapewa aina ya kazi za nyumbani-home work na msaada wa mafunzo zaidi katika maswali yanayowapa shida.
Ili wawe mastadi wakubwa wa keshokutwa,ndio shabaha ya chipukizi hawa wote kati ya umri wa miaka 15 na 16.
Mbali na ustadi wao wa kuzaliwa ,wanahitaji pia uwezo wa kujiamini na nidhamu ili kufaulu baadae.
Katika jumla la vijana la bayern munich, hakuna kijana chini ya umri wa miaka 15.Lakini, majira haya ya kiangazi taarifa moja kwa waandishi habari iligonga vichwa vya habari kuwa kuna kijana wa umri wa miaka 13 kutoka Paeru alieajiriwa na Bayern Munich kuceza dimba.Werner Kern,kiongozi wa jumba hilo la vijana anaeleza:
“Ilikua hivi :daktari mmmoja nchini Peru, alietaka mwanawe ajiunge na klabu moja mashuhuri kwa mafunzo ili aone upeo wa ustadi wake.Chipukizi huyo aitwae Pier Laraurri,anakwenda shule ya kimataifa tena kila siku mjini Munich kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 10 jioni.Na baadae, ndio anacheza kwetu mpira.”
Hakuna fedha zozote zilizolipwa kumleta Munich chipukizi huyo-asema Kern.
Kwa ufupi, klabu nyingi zinaamini “ulianza ufizi, ndipo yakaota meno”. Ukitaka kujua nguvu za timu ya taifa,angalia chipukizi wake.