Chuck Hagel aidhinishwa rasmi Marekani
27 Februari 2013Hagel aliidhinishwa kwa kura 58 dhidi ya 41, kufuatia kura nyingine iliyopigwa kukomesha makakati wa ucheleweshwaji wa uteuzi huo uliyoongozwa na wabunge wa chama cha Repulican. Wabunge wanne kutoka chama cha Republican waliungana na 52 wa Democrats na wawili wa kujitegemea katika kura ya ndio kwa uteuzi huo.
Ni ushindi dhidi ya makundi ya kiyahudi
Kura hiyo iliashiria kushindwa kwa wahafidhina wenye msimamo mkali, hususani kamati ya dharura ya Israel ECI na mwenyekiti wake Bill Kritol, ambaye jarida lake la Weekly Standard na mtandao vimekuwa vikichapisha mfululizo wa madai dhidi ya Hagel, kuanzia chuki dhidi ya wayahudi hadi uadui mkubwa dhidi ya Israel, tangu alipotangazwa kuwa chagua la rais Obama kwa nafasi hiyo kati kati ya mwezi Desemba.
Ni juhudi zisizo na mfano zilizogharimu mamilioni ya dola kumshinda mteule wa nafasi wa uwaziri, ikihusisha matangazo ya bei ghali ya kurasa nzima katika Jarida la Wall Street, na machapisho mengine pamoja na matangazo ya televisheni ya kumpinga Hagel katika majimbo muhimu. Wabunge wa chama cha Republican wanamtuhumu Hagel kwa kile wanachokiita msimamo wake laini kuhusu Iran, kupendelea zaidi kuondoa silaha za nyuklia za Marekani na kuwa na msimamo mkali dhidi ya Israel.
Hagel ambaye alijeruhiwa mara mbili wakati wa vita vya Vietnam, anaunga mkono mkakati wa rais Obama wa kumaliza vita nchini Afghanistan kufikia mwishoni mwa mwaka 2014, lakini vita vikubwa zaidi vinamsuburi atakapoanza kufanya kazi. Mablioni ya dola katika makato ya laazima ya bajeti yanatarajiwa kuanza Ijumaa wiki hii kama bunge halitasitisha makato hayo. Na hiyo itamaanisha makato ya dola bilioni 46 zitapunguzwa katika bajeti ya ulinzi katika miezi saba ijayo, na mamia ya wafanya kazi wa kiraia wanaweza kupoteza ajira zao kwa muda.
Kazi ngumu mbele yake
Rais Obama alikaribisha kuidhinishwa kwake kwa msingi usiyo wa vyama na kusema hatua hiyo inamuwezesha kuwa na waziri wa ulinzi ambaye taifa hilo linamhitaji, na kiongozi ambaye jeshi la Marekani linamhitaji. Ingawa wapinzani wake walishindwa kuzuia uteuzi wake mwishoni, wameashiria kuwa Hagel anaweza kuwa na wakati mgumu litakapokuja suala la kufanya kazi na bunge, bila kuwa na uungwaji mkono unaovuka mipaka ya vyama, ambao watangulizi wake walikuwa nao.
Ingawa Hagel alikuwa na msismamo wa kihafidhina wakati wa useneta wake, wenzake katika chama cha Republican hawajamsamehe kutokana na ukosoaji wake mkali, wa namna rais George Bush alivyoshughulikia vita vya Iraq, akiziita juhudi za utawala wake wakatihuo kuwa ni zaidi ya udhalili.
Lakini kuthibitishwa kwake ni ushindi mara mbili kwa rais Obama, ambaye waziri wake wa fedha Jack Lew pia alipita katika mchujo wakamati ya fedha ya seneti licha ya kuwepo na vinyongo kadhaa kuhusiana na sifa zake kama mdemokrati mnadharia mwneye uhusiano na wafanyiabiashara wa Wall Street.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe, ips, dpa.
Mhariri: Sekione Kitojo