1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chuck Hagel ziarani Misri

Admin.WagnerD24 Aprili 2013

Waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel ambaye anafanya ziara katika eneo la mashariki ya kati, amewasili nchini Misri leo hii. Ziara yake ina lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya Marekani na nchi za eneo hilo.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel
Waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck HagelPicha: Getty Images

Kabla ya kuzuru Misri, waziri Chuck Hagel amezitembelea Israel na Saudi Arabia, ambao ni washirika wakubwa wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati. Ziara yake ambayo ni ya kwanza mashariki ya kati kama waziri wa ulinzi wa Marekani, inadhamiria kuimarisha ushirikiano baina ya nchi yake na mataifa ya eneo hilo katika kukabiliana na ushawishi wa Iran na kuzuia kuenea kwa siasa kali za kiislamu.

Mjini Cairo, bwana Hagel anafanya mazungumzo na mwenzake wa Misri Jenerali Abdel Fattah al-Sissi, na baadaye atakutana na rais wa nchi hiyo Mohammed Morsi.

Misri bado ni muhimu kwa Marekani

Kwa miongo kadhaa Misri ilikuwa kitovu cha mikakati ya Marekani katika eneo la mashariki ya kati, lakini tangu kuangushwa kwa utawala wa rais Hosni Mubarak mwaka 2011, Marekani imekabiliana na hali mpya kisiasa nchini humo, inayoongozwa na watu wanaozingatia zaidi uhuru wao kifikra.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry akiwa na Rais wa Misri Mohammed Morsi mjini Cairo hivi karibuniPicha: picture-alliance/dpa

Licha ya hayo lakini, maafisa wa Marekani wanasema kuwa ushirikiano wa kijeshi na nchi hiyo uliojengwa kwa miaka mingi bado upo, na kwamba viongozi wa jeshi la Marekani bado wanayo mawasiliano ya moja kwa moja na makamanda wakuu wa jeshi la Misri.

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuanza kwa ziara ya Chuck Hagel, afisa mwenye cheo cha juu katika wizara ya ulinzi ya Marekani alisema kuwa hadi sasa, waziri wa ulinzi wa Marekani anaweza kuzungumza kwa simu na mwenzake wa Misri wakati wowote.

Msaada wa kijeshi waendelea

Hata baada ya kuangushwa kwa utawala wa Hosni Mubarak, Marekani imeendelea kuipa Misri msaada wa kijeshi wenye thamani ya dola bilioni mbili kila mwaka. Msaada huo unatazamwa kama nyenzo ya kuifanya Misri iendelee kuheshimu makubaliano ya amani kati yake na Israel, ambayo yalitiwa saini mwaka 1979.

Misri na Israel zilisaini mkataba wa amani mwaka 1979Picha: AP

Maafisa wa pande mbili wamesema kuwa wakati wa ziara yake nchini Misri, Chuck Hagel atazungumza na viongozi wa nchi hiyo kuhusu uhusiano na Israel, kuzorota kwa usalama katika eneo la Sinai, na pia siasa za ndani za Misri.

Ziara ya waziri huyo wa ulinzi wa Marekani imefanywa wakati Misri ikikabiliwa na mgogoro wa kisiasa, matatizo ya kiuchumi, pamoja na upinzani ambao unatishia kususia uchaguzi wa bunge.

Ingawa lengo kubwa la ziara ya bwana Hagel mashariki ya kati lilikuwa kuimarisha ushirikiano wa kijeshi, suala la vita vinavyoendelea nchini Syria ambako serikali ya nchi hiyo inashutumiwa kutumia silaha za sumu, pia limechukua kipaumbele.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/APE

Mhariri:Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW