1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

'Chuki dhidi ya Wayahudi inaongezeka tena ulimwenguni'

18 Januari 2023

Kiongozi wa makumbusho ya Mauaji ya Wayahudi ya Yad Vashem huko Israel Dani Dayan anazuru Ujerumani kwa mara ya kwanza maishani mwake na kuzungumza na DW kuhusiana na ziara hiyo na vita vya chuki dhidi ya Wayahudi.

Dani Dayan Vorstandsvorsitzender der Gedenkstätte Yad Vashem
Picha: Alex Kolomoisky/Yad Vashem

Dani Dayan mwenye miaka 67 anaiambia DW, ni bahati mbaya kwamba chuki dhidi ya Wayahudi inarejea tena ulimwenguni. Anasema katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu hivi, amekuwa mwenyekiti wa makumbusho ya Yad Vashem, ambayo umaarufu wake ni kumbukumbu ya matukio ya chuki dhidi ya Wayahudi. Makumbusho hayo yanapatikana katika Mlima wa Kumbukumbu uliopo mjini Jerusalem.

Dayan amemwambia Rebecca Ritters wa DW kwamba ongezeko la visa vya chuki dhidi ya Wayahudi ni kitu kinachomsukuma kumuonya kila kiongozi ulimwenguni anayezuru makumbusho hayo, akiwaambia kila wanapoona visa hivyo wachukue hatua mara moja badala ya kusubiri. Anasema wanaposubiri chuki hiyo itaongezeka na kuwa kitu kikubwa ambacho itakuwa vigumu kukizuia siku za usoni.

Januria 22, Dayan atazuru Ujerumani kwa mara ya kwanza maishani mwake. Ni historia ndefu. Alizaliwa Argentina mwaka 1955 na kuishi huko hadi familia yake ilipohamia Israel mwaka 1971. Alikulia Israel na hatimaye kuwa mmoja ya viongozi wa kisiasa wa vuguvugu la makazi la Israel katika eneo la Ukingo wa Magharibi. Tangu alipoteuliwa kuwa mkuu wa Yad Vashem, Dayan anasema amejitenga kabisa na masuala ya siasa.

Dani Dayan akizungumza na mwandishi wa DW Rebecca RittersPicha: Tania Kraemer/DW

Alipokuwa mdogo, Dayan aliapa kutokanyaga Ujerumani, mahali ambako kuna wahusika wa mauaji ya Wayahudi. Lakini hata hivyo, anasema kwa sasa haoni sababu ya kuwa na chuki na badala yake, anachozingatia kwa sasa ni kutoa heshima kwa Wayahudi milioni sita waliouawa.

Soma Zaidi: Kikongwe wa miaka 97 ahukumiwa kwa mauaji ya wakati wa vita vya pili vya dunia

Jihadharini na kuibuka kwa visa vya chuki.

Ingawa ulimwengu umeshuhudia kuongezeka kwa matukio ya chuki, Dayan anasisitiza juu ya utofauti kati ya ulimwengu wa leo na wa miaka ya 1930, wakati vuguvugu la National Socialist lililoongozwa na Adolf Hitler lilipokuwa likijiimarisha nchini Ujerumani na kusababisha mauaji makubwa ya Wayahudi waliokuwepo Ulaya. Hata hivyo anasema ulimwengu hauko mbali sana na wakati huo, ingawa tofauti na jamii ya wakati huo, watu hii leo wanajua kile kinachoweza kutokea, ikiwa kitakuwa kimeanzia kwenye mazingira mabaya.

Mkutano wa kwanza kwenye makumbusho ya Yad Vasham

Ziara hii ya Dayan inafuatia mwaliko kutoka kwa rais wa bunge la shirikisho la Ujerumani, Bundestag, Bärbel Bas aliyezuru Israel mwezi Aprili mwaka 2022. Alikuwa afisa wa kwanza wa ngazi za juu wa Ujerumani kushiriki maadhimisho ya kila mwaka ya kumbukumbu ya mauaji ya Wayahudi katika bunge la Israel, Knesset, ambako majina ya wahanga husomwa kwa sauti. Lakini pia alitembelea makumbusho hayo.

Bäbel Bas akiweka taji la maua katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Holocaust, mjini Jerusalem mwaka uliopita.Picha: AMIR COHEN/picture alliance

'Chuki dhidi ya Wayahudi inaongezeka tena ulimwenguni'

Ni kufuatia ziara kwenye akumbusho hayo, ndipo Bas alimwalika Dayan kufungua maonyesho kwenye bunge la Ujerumani mjini Berlin kuelekea siku ya kimataifa ya kumbukumbu ya Mauaji ya Wayahudi Januari 27. Kwa pamoja watazungumza katika ufunguzi wa maonyesho hayo Januari 24 na yaliyopewa jina "Vifaa 16-Miaka 70 ya Yad Vashem." Maonyesho haya yatafanyika katika moja ya jengo la Bundestag la Paul Löbe.

Maonyesho hayo yatahusisha vifaa 16, miongoni mwa vile vilivyopo kwenye makumbusho ya Yad Vashem, pamoja na shuhuda za maisha ya kila siku ya Wayahudi waliolazimika ama kuondoka Ujerumani au kubaki na kuuliwa na waNazi.

Soma Zaidi: Auschwitz - mahali penye historia ya kutisha

Hii leo idadi ya manusura wa mauaji hayo ya Wayahudi inazidi kupungua. Ni wazee wachache wanaoweza kukiambia kizazi cha sasa kile kilichotokea huko nyuma. Na Dayan anaanza kuangazia itakavyokuwa wakati manusura hawa wote watakapoondoka. Anasema ni wazi kwamba kazi yao itakuwa ngumu zaidi lakini pia itakuwa muhimu zaidi, kwa kuwa anasema utakuwa ni wakati wa furaha na hasa kwa wapotoshaji waliopo hii leo na kuongeza kuwa hiyo ni moja ya sababu inayoashiria kwamba wako nyuma ya muda.

Kwenye ziara hii, Dayan atakaa kwa siku mbili mjini Berlin lakini pia amepangiwa kukutana na rais wa shirikisho la Ujerumani Frank-Walter Steinmeir na kansela Olaf Scholz, waziri wa fedha Christian Lindner, wanachama waandamizi wa Chama cha Kijani na kiongozi wa upinzani kutoka chama cha Christian Democratic Union, CDU Friedrich Merz. Atatembelea pia Makumbusho ya Wayahudi wa Ulaya waliouawa ya mjini Berlin, Makumbusho ya Wayahudi na wanachama wa jamii ya Uyahudi ya mjini Berlin.

Soma Zaidi: Dunia yaadhimisha mauaji ya halaiki ya Holocaust

Mwandishi: Christoph Strack

Mtafsiri: Lilian Mtono

Mhariri: Zainab Aziz