1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CITES yafikia makubaliano ya kuwalinda ndovu

Caro Robi
7 Oktoba 2016

Mkutano wa kimataifa kuhusu viumbe walio katika hatari ya kuangamia umemalizika Johannesburg kwa maafikiano ya kudhibiti biashara haramu ya wanyama kadhaa wakiwemo wasio maarufu, kama kakakuona na papa.

Botswana Afrikanische Elefanten mit einem toten Artgenossen
Tembo wa Botswana wakimtazama mwenzao aliyeuawaPicha: picture alliance/WILDLIFE/M. Harvey

Licha ya kuwepo tofauti kali wakati wa mkutano huo ambao nchi za Afrika zilizishutumu nchi za magharibi kwa kile zilichokitaja kuwaamulia jinsi ya kuwalinda ndovu wao, wanaharakati wamesifu hatua zilizochukuliwa katika mkutano huo za kuwalinda wanyama na mimea iliyo katika hatari ya kuangamia.

Mgongano kuhusu mauzo ya pembe za ndovu

Muungano wa nchi 29 za Afrika zikiongozwa na Kenya na Benin zilitaka ndovu wa Afrika kuwekwa katika kiwango cha kwanza cha mkataba wa CITES ambapo biashara zote za pembe za ndovu zitapigwa marufuku. 

Hata hivyo Afrika Kusini, Namibia na Zimbabwe zilipinga marufuku hiyo zikisema zinapaswa kuruhusiwa kuendelea kuuza mrundo wa pembe ilizonazo kwani wana idadi ya kutosha na inayokua ya tembo.

Awali, katika mkutano huo wa CITES asilimia kubwa ya nchi 180 zilizohudhuria zilipiga kura kupinga mapendekezo ya Namibia na Zimbabwe ya kuuza pembe zake zilizotokana na wanyama kufariki kifo cha kawaida na zilizonaswa kutoka kwa wawindaji haramu ili kufadhili miradi ya jamii zinazoishi karibu na mbuga za wanyama pori.

Shehena ya pembe za ndovu katika Hifadhi ya Taifa ya Zimbabwe.Picha: picture-alliance/AP Photo/T. Mukwazhi

Wajumbe pia walipinga pendekezo la Swaziland la kutaka kuruhusiwa kuuza pembe zake za faru tangu kuzuiwa kufanya hivyo 1977 kufuatia marufuku ya kimataifa.

Licha ya kupungua kwa ndovu na faru, bado yapo matumaini

Idadi ya ndovu Afrika imepungua hadi 415,000 tangu uwindaji haramu ulipoongezeka mwaka 2006 huku idadi ya faru waliowindwa waliouliwa Afrika Kusini pekee ikiongezeka kutioka 13 mwaka 2007 hadi 1,175 mwaka jana.

Mkuu wa CITES John Scanlon amesisitiza jumuiya ya kimataifa imepiga hatua kubwa katika kuwalinda viumbe walio katika hatari akiutaja mkutano huo kama uliobadili mkondo kuhusu hatma ya wanyama na mimea iliyo katika hatari ya kuangamia.

Biashara ya pembe za ndovu na faru zimepigwa marufuku kimataifa tangu 1989 lakini licha ya marufuku hiyo, biashara haramu ya pembe za wanyama hao walio katika hatari ya kuangamia imeendelea katika nchi kadhaa za Afrika.

CITES iliruhusu uuzaji wa mrundo wa pembe hizo kutoka Afrika kwa nchi za Japan na China mwaka 1999 na 2008. Biashara haramu ya wanyama pori inakadiriwa kuwa ya thamani ya dola bilioni 20 kwa mwaka. Mkutano huo wa kimataifa kuhusu viumbe vilivyo katika hatari ya kuangamia huandaliwa kila baada ya miaka mitatu na mkutano ujao utafanyika Sri Lanka mwaka 2019.


Mwandishi: Caro Robi/afp
Mhariri: Gakuba Daniel

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW