1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Clinton asema shutuma za Rais Assad kwa nchi za nje ni unafiki

Admin.WagnerD12 Januari 2012

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hilary Clinton amesema shutuma za Rais wa Syria kuwa nchi za nje zina njama dhidi ya nchi yake, ni unafiki mkubwa.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hilary Clinton anasema kauli ya Rais Assad ni unafiki
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hilary Clinton anasema kauli ya Rais Assad ni unafikiPicha: AP

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Washington, Hilary Clinton amesema kile kinachosikika kutoka kwa Rais Bashar al Assad ni unafiki wa kutisha, na kutoa lawama kwa nchi za nje kama kisingizio. Matamshi haya ya Clinton yanafuatia ujumbe uliotolewa na Rais Bashar al Assad jana baada ya kushiriki katika maandamano ya kuunga mkono serikali yake ambayo yalifanyika katika mji wenye machafuko mengi wa Homs.

Akisindikizwa na mke wake Asma, Rais Bashar al Assad alizishutumu nchi za kigeni kwa kile alichokiita njama dhidi ya Syria, na kutabiri kwamba njama hizo zitashindwa katika siku za hivi karibuni. Aliwashukuru waandamanaji wanaomuunga mkono, na kusema anatiwa nguvu na ujasiri wao.

Rais wa Syria Bashar al Assad anadai machafuko nchi mwake yanasababishwa na njama kutoka njePicha: AP

Katika maandamano hayo waliuawa watu saba, akiwemo muandishi wa habari kutoka Ufaransa Gilles Jacquier. Marekani ilisema kuuawa kwa mwandishi huyo kumetokana na kukosekana kwa mazingira salama kwa waandishi nchini Syria.

Serikali ya mjini Damascus imewashutumu wale iliowaita magaidi wenye silaha kwa mauaji hayo ya jana, na kuahidi kuwa itafanya kila linalowezekana kuwakata mikono magaidi hao. Shirika la habari la nchi hiyo SANA limeikariri wizara ya habari ya Syria ikisema imesikitishwa na kifo cha mwandishi huyo.

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy ameihimiza Syria kufanya uchunguzi wa kina na wa haraka, kubainisha chanzo cha mauaji ya mwandishi huyo, ambaye amesema aliuawa akijaribu kutekeleza wajibu wake. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza Wiliiam Hague na mkuu wa sera wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton pia wameshutumu mauaji ya mwandishi huyo.

Gilles Jacquier, mwandishi wa habari aliyeuawa nchini SyriaPicha: dapd

Kulingana na taarifa ya kundi la haki za binadamu la Syrian Observatory for Human Rights, roketi ilivurumshwa katika mitaa ya Akrama na Al-Nuzha ambako kulikuwa na kundi la waandishi wa habari 15 kutoka nchi za magharibi ambao walikuwa wamealikwa na serikali kufuatilia maandamano yanayoiunga mkono. Kundi hilo halikusema nani alirusha roketi hiyo.

Katika maandamano hayo ya jana, Rais al Assad alisema ushawishi kutoka nchi za kikanda na za mbali ambao unajaribu kuiyumbisha nchi hauwezi kuamua mkondo wa mambo ndani ya Syria.

Kauli yake hiyo ilichukuliwa na wapinzani kama msimamo wa kuisukuma nchi kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Mwenyekiti wa baraza la kitaifa la Syria lenye makao yake nchini Uturuki, Burhan Ghaliouni alisema matamshi ya Bashar al Assad yalikuwa ya hatari ambayo yanaonyesha dhamira yake kutumia mabavu kuukandamiza upinzani.

Mwandishi: Daniel Gakuba/DPA/AFPE

Mhariri:Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW