Clinton awasifu wanaharakati nchini Uganda
4 Agosti 2012Clinton ameutunukia muungano wa makundi ya haki za binadamu nchini Uganda tuzo ya wizara ya mambo ya kigeni ya mwaka 2011 ya utetezi wa haki za binadamu , ambayo ni ishara kwa mataifa ya Afrika na ya Kiislamu kuwa Marekani haitarejea nyuma katika mapambano yake dhidi ya ukandamizaji wa kisiasa na kisheria dhidi ya mashoga.
Ni muhimu kwa Waganda , serikali na raia kwa pamoja , kukemea dhidi ya ukandamizaji, unyanyasaji, pamoja na kutishwa kwa mtu yeyote. Hii ni kweli kwa mtu yeyote hata kama anatoka wapi, wanaimani gani, ama wanampenda nani, Clinton amesema.
Clinton amesema kuwa amelizusha suala hilo katika mazungumzo siku ya Ijumaa na rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni, ambaye serikali yake imekuwa ikishutumiwa kwa kuruhusu viongozi wa kidini na kisiasa kupigia upatu hisia dhidi ya mashoga katika nchi hiyo ya kihafidhina ya Afrika mashariki.
Mfano kwa wote
Nyie ni mfano kwa wengine na mfano kwa dunia, Clinton amewaambia wawakilishi wa kundi, lililoundwa mwaka 2009 kupambana na mswada wa sheria ambao unapendekeza adhabu ya kifo kwa yeyote atakayehukumiwa kwa kosa la ushoga.
Mswada huo , ambao ulizusha shutuma kali duniani, ulikwama bungeni lakini umerejeshwa tena katika umbo ambalo limetoholewa na kuwasilishwa na mwanachama wa chama cha Museveni.
Mswada huo mpya umeondoa kipengee cha adhabu ya kifo, lakini bado unalenga katika kufanya kinyume na sheria kupigania haki za mashoga, na kumuadhibu yeyote ambaye atachangia kwa fedha, kufadhili ama kusaidia ushoga.
Hatua ya Clinton ya kuonyesha mshikamano na jamii inayonyanyaswa ya mashoga nchini Uganda inakuja wakati anaendelea na ziara yake ya mataifa saba katika bara la Afrika.
Siku ya Ijumaa alifanya ziara katika taifa jipya la Sudan kusini, ambako aliitaka serikali mpya ya nchi hiyo mjini Juba kufanya makubaliano na watawala wao wa zamani Sudan ya kaskazini ili kutatua mzozo unaohusiana na mapato ya mafuta, hali ambayo imesababisha mataifa yote kuingia katika mkwamo wa kiuchumi.
Kony atasakwa kwa ndege
Uganda ambayo ni mshirika mkubwa wa Marekani katika masuala ya usalama , imechangia kwa kiasi kikubwa jeshi la umoja wa Afrika nchini Somalia na Clinton amesema kuwa ndege zisizo na rubani huenda zikatumika kuisaidia Marekani na Uganda katika juhudi zake za pamoja kumsaka kiongozi wa kundi la LRA Joseph Kony.
Leo Jumamosi (04.08.2012) anakwenda nchini Kenya, kabla ya kuendelea na safari hadi Malawi na Afrika kusini.
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre
Mhariri : Bruce Amani.