1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Clinton kukutana na Rais Sirleaf wa Liberia

Kabogo Grace Patricia13 Agosti 2009

Clinton amesema anaunga mkono jitihada za rais pekee mwanamke Afrika.

Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf.Picha: picture-alliance/dpa

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton leo anatarajiwa kukutana na Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf, katika jitihada za kumuunga mkono rais pekee mwanamke barani Afrika. Wakati wa ziara yake kwenye mataifa saba barani Afrika, Bibi Clinton amekuwa akisisitiza juu ya kuwezeshwa kwa wanawake. Grace Kabogo na taarifa zaidi:

Baada ya mikutano kadhaa na kuhudhuria shughuli za kijamii nchini Nigeria, Bibi Clinton hii leo atakuwa na mazungumzo na Rais Sirleaf, ikiwa ni kituo chake cha sita katika ziara yake hiyo ya siku 11. Bibi Sirleaf amekuwa akiungwa sana mkono na nchi za Magharibi, hasa Marekani, ambapo anaendeleza jitihada za kuijenga upya nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Johnnie Carson, Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje kwa masuala ya Afrika, amesema Bibi Clinton anataka kuonyesha uungaji mkono kwa Rais Sirleaf.

Hata hivyo, hivi karibuni Tume ya Ukweli na Maridhiano ya Liberia, ilimzuia Rais huyo wa Liberia, kushiriki katika shughuli za kisiasa kwa miaka 30 kwa tuhuma za kuhusika katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo kati ya mwaka 1989 na 2003.

Bibi Clinton ameitumia ziara yake hiyo kuzungumzia haki za msingi za wanawake kwa kutembelea eneo lililoharibiwa kwa vita la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo la Goma kuwafariji wanawake waliobakwa, ambapo aliitaka nchi hiyo kuongeza juhudi kuhakikisha mwanamke wa Afrika anatambuliwa. Bibi Clinton anasema:

'' Nimekutana na Rais Kabila na nimemwambia tunataka kusaidia kumaliza vurugu ili muweze kwenda nyumbani.''

Akizungumza katika mahojiano nchini Nigeria, Bibi Clinton alisema hakuna nchi inayoweza kupata maendeleo kamili bila ushiriki wa mwanamke. Amesema kama wanawake wa Afrika wakiacha kufanya kazi, dunia nzima itafungwa, kwa kuwa mazao hayatapandwa na watu hawatakula.

Aidha, Waziri huyo wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani aliitaka Nigeria kuwa na utawala bora, kumaliza tatizo la rushwa na kuonya kuwa rushwa inaweza ikarudisha nyuma uchumi wa nchi hiyo. Akiongeza, Bibi Clinton anasema:

''Maendeleo yanategemea sana utawala bora na utawala wa kuheshimu sheria. Hilo linapunguza mazingira ya uwekezaji pamoja na ukuaji wa uchumi.''

Bibi Clinton pia aliitaka Nigeria kuimarisha uhusiano wa kibiashara na uwepo wa uvumilivu baina ya Wakristo na Waislamu.

Baada ya kutoka nchini Liberia, Bibi Clinton atamalizia ziara yake hiyo nchini Cape Verde, kabla ya kurejea nchini Marekani kesho Ijumaa. Ziara yake hiyo ilizihusisha pia nchi za Kenya, Afrika Kusini na Angola.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE/AFPE)

Mhariri:M.Abdul-Rahman