1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Clinton na Trump waendelea kukabana koo dakika za majeruhi

Sylvia Mwehozi
1 Novemba 2016

Wagombea urais wa Marekani Hillary Clinton wa Democrats na Donald Trump wa Republican wameendelea kurushiana maneno na kukabana koo katika dakika za lala salama za kampeni zao.

USA Bildkombo Hillary Clinton und Donald Trump
Picha: Getty Images/AFP/B. Smialowski/J. Swensen

Clinton ameonya kwamba Trump hafai kupewa udhibiti wa namba za siri za nguvu za nyuklia huku Trump mwenyewe akiendelea kumwandama mpinzani wake juu ya usiri uliogubika matumizi ya barua pepe binafsi zikiwa zimesalia siku saba kabla ya uchaguzi kufanyika. Ikiwa ni dakika za majeruhi katika mbio za kuelekea Ikulu ya Rais hapo Novemba nane katika uchaguzi wa rais, Trump anaonekana kutumia taarifa za uchunguzi mpya wa shirika la upelelezi la Marekani FBI juu ya Bi Clinton kutumia anuani binafsi ya barua pepe wakati alipokuwa waziri wa mambo ya nje.

Lakini pasipo na ishara ya shirika hilo kuja na matokeo kamilifu ya uchunguzi huo kabla ya siku ya kupiga kura, Clinton anaamini kwamba ataendelea kukabiliana na Trump na hasa suala la udhibiti wa nguvu za nyuklia.

Bi Hillary Clinton katika moja ya kampeni zakePicha: picture-alliance/dpa/J. Lo Scalzo

Akiwa mjini Ohio, Clinton anasema Trump hapaswi kuaminiwa kupewa namba za siri za nguvu za nyuklia. Clinton akimzungumzia Trump namna alivyokuwa akijibu maswali ya kiusalama, anasema mgombea huyo ni hatari na ambaye anaweza kuchochea vita. Kuhusu uchunguzi mpya wa barua pepe binafsi Clinton anaamini majibu yatakuwa ni yale yale.

"Ninaamini wengi wenu mnajiuliza hadithi hii mpya ya barua pepe inahusu nini, na kwanini FBI waingilie uchaguzi bila ya kuwa na ushahidi wa makosa yoyote, ikiwa zimebaki siku chache tu. Hilo ni swali zuri. Na kwanza kabla ya yote niseme kwa wote ambao mna wasiwasi juu ya mimi kutumia anuani binafsi ninawaelewa na kama nilivyosema siwezi kuhalalisha hilo. Nilishasema kwamba nilifanya makosa na najua hilo. Hakuna kesi hapa " alisema Bi Clinton. 

Trump kwa upande wake ameendelea na shutuma zake dhidi ya matumizi ya anuani ya barua pepe binafsi ambayo anadai kwamba yanaiweka Marekani katika hatari na kusema mpinzani wake hana uzoefu kama anavyojinasibu. Trump ameendelea na kampeni zake mjini Michigan na kuweka mkazo wa mashambulizi katika uchunguzi mpya wa FBI.

Donald Trump aksisitiza jambo katika mojawapo ya kampeni zakePicha: picture-alliance/dpa/G. He

Trump amenukuliwa akisema kwamba "hii ni kashfa kubwa tangu ile ya watergate. Hillary Clinton anataka kumlaumu kila mtu kwa kusababisha matatizo ya kisheria, lakini hili amelitengeneza mwenyewe na hapaswi kumlaumu mtu yeyote. Hillary ni yeye aliyetuma na kupokea taarifa za siri kupitia akaunti isiyo salama na kuweka usalama wa wamarekani chini ya kitisho."

Hata hivyo utafiti wa kura za maoni uliofanywa baada ya kauli ya FBI siku ya Ijumaa umeonyesha mabadiliko kidogo dhidi ya Trump ikiwa imesalia wiki moja kabla ya uchaguzi. Licha ya kashfa hiyo ya barua pepe, bado Bi Clinton anaongoza kwa umaarufu japo kwa asilimia ndogo.

Madai ya kwamba Clinton aliiweka Marekani katika hatari kwa kutumia anuani binafsi yaliibuliwa tena baada ya mkurugenzi wa FBI James Comey kusema kwamba watachunguza uwepo wa barua pepe mpya kama zinamhusu Clinton na kuona kama zilikuwa na taarifa ya siri.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri : Caro Robi

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW