1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Clinton ziarani Indonesia.

Halima Nyanza/DPA18 Februari 2009

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hillary Rodham Clinton ameahidi nchi yake itakuwa na uwazi na kupokea fikra mpya, hususan kutoka ulimwengu wa Kiislamu. Bibi Clinton amesema hayo leo nchini Indonesia.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Rodham Clinton, akiwa ziarani nchini Indonesia.Picha: AP

Akizungumza leo nchini humo katika mkutano na waandishi wa habari ambao pia ulihudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Indonesia Hassan Wirajuda, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton alisema anataka kuonesha kuunga mkono kwake sio tu demokrasia iliyopatikana kwa shida nchini humo, bali pia mafanikio ya nchi hiyo katika juhudi za kupambana na ugaidi, wakati huohuo ikiheshimu haki za binadamu.


Amesema uhusiano wa nchi yake na Indonesia, nchi ambayo ina idadi kubwa ya waumini wa kiislamu ni muhimu hususan katika juhudi za Marekani kurekebisha uhusiano wake na mataifa ya kiislamu.


Aidha Waziri wa Mambo ya nchi za Nje wa Marekani amesema Indonesia ni nchi ambayo imethibitisha kuwa dini ya kiislamu na demokrasia vinaweza kuchanganywa.


Bibi Clinton amesema pia juhudi zimeanza kuchukuliwa ili kuimarisha uhusiano na kuashiria kupatikana na misaada ya maendeleo.


Ameongezea kuwa kutokana na uhakika kuwa Indonesia ni nchi yenye waislamu wengi duniani na nchi ya tatu kubwa kidemokrasia, itatoa mchango mkubwa katika kuendeleza mustakabali wa pamoja wa nchi hizo.


Katika ziara yake hiyo nchini Indonesia, Bibi Clinton na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje ya nchi hiyo Hassan Warajuda walijadiliana masuala mbalimbali katika kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili, ambapo Bibi Clinton alisema jambo la kwanza marais wa nchi hozo mbili wanaazma ya kuwa na mpango wa ushirikiano maalum utakaoshughulikia masuala yanayohusu kila nchi na pia masuala ya kikanda na ya kimataifa, utakaohusisha hatua za kulinda mazingitra na kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa, biashara, uwekezaji, kuimarisha demokrasia, afya na elimu na usalama wa kikanda pamoja na ugaidi.


Marekani ni nchi ya pili ambayo Indonesia imekuwa ikisafirisha bidhaa zake, lakini Indonesia imekuwa ikikosoa baadhi ya sera za nchi hiyo wakati wa uongozi wa Rais aliyemaliza muda wake George W Bush.


Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani anafanya ziara ya siku mbili nchini Indonesia yenye lengo la kuonesha wajibu wa ahadi alizozitoa Rais Barack Obama katika sera mpya za nchi hiyo ikiwa ni pamoja kuimarisha uhusiano wa nchi yake na mataifa ya kiislamu.


Ulinzi umeimarishwa nchini humo hususan katika mji mkuu wa Jarkata kwa jeshi na polisi kujiweka katika hali ya tahadhari katika mitaa mikubwa ya mji huo,Kulifanyika mikutano ya kupinga ujio wake lakini ilikuwa midogo.







Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW