Clinton ziarani Sudan Kusini
3 Agosti 2012Hii ni ziara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi za ju wa Marekani tangu Sudan ya Kusini ipate uhuru wake mwaka jana. Kando na mkutano wake na Rais Salva Kiir, Clinton atakutana pia na waziri mwenziwe wa mambo ya nje, Nhial Deng Nhial.
Afisa wa ngazi ya juu wa Marekani ambaye ameambatana na Clinton amesema kuwa nchi yake inaunga mkono juhudi za kupatikana muafaka baina ya Sudan na Sudan ya Kusini.
Akionyesha namna ambavyo nchi yake iko pamoja na Sudan ya Kusini, afisa huyo amesema "Clinton ataeleza kwa kina juu ya wasiwasi tulionao kuhusu kutokusonga mbele kwa makubaliano na vipengele muhimu vilivyotumika kuitenganisha Sudan na Sudan ya Kusini."
Alifafanua kuwa vipengele hivyo ni masuala ya mafuta, mgawanyo wa mapato, uraia na mzozo wa mpaka, na kusema kuwa nchi zote mbili zinakabiliwa na utengaji mbaya wa fursa za kiuchumi.
Lengo la ziara ya Clinton Afrika
Shabaha ya ziara hiyo ya siku 11 ya Clinton barani Afrika, ni kutimiza mpango mkakati mpya wa utawala wa Rais Barack Obama barani humo. Mkakati huo unahusisha ukuzaji wa maendeleo kwa kuchochea ukuzaji wa uchumi pamoja na kuimarisha hali ya amani, usalama na demokrasia.
Serikali ya Sudan ya Kusini inakabiliwa na kibarua cha kumaliza mzozo baina yake na Sudan ambao umeachwa bila ya utatuzi tangu Sudan ya Kusini ilipojitenga mwezi Julai mwaka jana.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa muda wa hadi siku ya jana kwa mahasimu hao kufikia muafaka ama wakabiliane na vikwazo. Muda huo umepita bila ya makubaliano yoyote.
Mkutano wa Baraza la Usalama na Amani la AU
Kutokana na hali hiyo, Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika linakutana leo na pande zote mbili mjini Addis Ababa, Ethiopia kwa mazungumzo. Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki amekuwa akiongoza mazungumzo ya amani baina ya mataifa hayo chini ya Umoja wa Afrika.
Kumekuwa na dhana tofauti juu ya mzozo huo hasa linapokuja suala la vikwazo. wapo wanoamini Sudan kusini haipaswi kuchukuliwa hatua hiyo kama Bwana Ojwang Katuku wa Nairobi nchini Kenya ambaye amekuwa akifuatilia mzozo huo kwa kina.
"Kwa upande wa Sudan itakuwa ni ishara kwa utawala wa Khartoum kwamba wasiwasi wa jumuiya ya kimataifa utakuwa na maana Fulani. Kuiwekea vikwazo sudan kusini haitakuwa sahihi kwa sababu jumuiya ya kimataifa itakuwa inamuweka mkosaji na mkosewa kwenye mstari mmoja." alisema Katuku.
Hata hivyo wanadiplomasia wanaofutailia mzozo huo wanasema kuwa hali ni tete sana. Wiki hii, Rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir alikataa kukutana na Rais Kiir kwa mazungumzo mjini Addis Ababa katika dakika za mwisho.
Mwandishi: Stumai George/AFP/AP
Mhariri: Mohammed Khelef