1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Colombia yaelekea kwenye duru ya pili ya uchaguzi

Daniel Gakuba
28 Mei 2018

Nchini Colombia, mgombea wa chama cha kihafidhina Ivan Duque ameshinda duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais iliyofanyika jana Jumapili, lakini hakupata asilimia 50 ambaye ingemwezesha kuepuka duru ya pili.

Kombo Kolumbien Stichwahl - Gustavo Petro und  Ivan Duque
Gustavo Petro (kushoto) na Ivan Duke ambao wamefuzu kuingia duru ya pili ya uchaguzi

Ivan Duque amepata asilimia 39.2 ya kura zote zilizopigwa, akifuatiwa katika nafasi ya pili, na mtu ambaye siku za nyuma alikuwa mwanachama wa kundi la waasi, Gustavo Petro aliyejishindia asilimia 25 ya kura. Uchaguzi wa jana Jumapili ni wa kwanza kufanyika bila kitisho cha waasi wa FARC katika kipindi cha takriban nusu karne. Uitikiaji wa wapigakura ulikuwa wa kiasi cha asilimia 53.2, na umefanyika katika mazingira ambayo mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi Juan Carlos Galindo ameyataja kuwa ya ''kawaida kabisa.''

Mazingira hayo ya amani yamesifiwa na Rais Juan Manuel Santos anayemaliza muda wake, ingawa makubaliano ya amani aliyoyasaini na kundi la waasi la FARC, yalikuwa kigezo kilichowapa mafanikio wagombea wawili waliofanikiwa kuingia duru inayofuata.

Kuyaandika upya makubaliano ya amani

Shamra shamra miongoni mwa wafuasi wa mhafidhina Ivan Duke aliyekuja katika nafasi ya kwanzaPicha: picture-alliance/AP/F. Vergara

Ivan Duque ameshinda kupitia jukwaa la ahadi ya kuyaandika upya makubaliano hayo, ambayo anasema yanaliendekeza sana kundi la FARC, ambalo liliendesha vita vya uasi kwa miongo kadhaa kabla ya kujigeuza kuwa cha cha siasa. Hata hivyo, amesema nia yake sio kuyasambaratisha makubaliano hayo.

''Hatuna mpango wa kuyavunja makubaliano ya amani'', amesema Duque na kuongeza kuwa wanachotaka kusema wazi ni kwamba ikiwa wanataka amani nchini Colombia, amani hiyo inapaswa kuandamana na haki, ''kwa kuzungumza ukweli, kuwalipa fidia wahanga, na kwa wafalifu kukamilisha vifungo vyao jela kulingana na matarajio ya wahanga.''

Gustavo Petro wa chama cha mrengo wa kushoto aliyekuja katika nafasi ya pili, ni mgombea wa kwanza wa mrengo huo kufanikiwa kuingia katika duru ya mwisho, ambayo kwa muda mrefu nchini Colombia imekuwa kinyang'anyiro kati ya vyama vya mrengo wa kulia. Mpiganaji huyom wa zamani wa kundi la M-19 amepata kura milioni 4.8, ambazo ni mara mbili ya alizozipata mgombea wa mwisho wa kambi ya kisoshalisti aliyefanya vyema katika uchaguzi wa mwaka 2006.

Wahafidhina wamecheza karata ya mwisho ?

Tume ya uchaguzi imesema zoezi limeendeshwa katika mazingira ya kawaida kabisaPicha: Getty Images/AFP/L. Robayo

Akuzumza na wafuasi wake baada ya matokeo kutangazwa, Petro amesema wananchi wa Colombia wanayo kiu ya mafanikio, na kubashiri kuwa watashinda, akidai upande wa Ivan Duke umecheza karata yake ya mwisho.

Amesema,  ''Nguvu zilizompa msukumo wa kuingia duru ya pili Ivan Duke, miongoni mwake mkuu wa zamani wa polisi na Rais wa zamani Alvaro Uribe zinaonekana kufika kikomo chake. Lakini kwa upande wetu, nguvu ya raia walio huru haina kikomo. Tunasonga mbele kwa hatua imara zaidi. Tunao uhakika kwamba tutashinda, na kuibadilisha historia ya Colombia.''

Mchambuzi wa siasa za Colombia Andres Macais ametabiri kuwa kampeni za duru ya pili zitakuwa zenye mgawanyiko mkubwa, huku kila mgombea akijaribu kuwavutia upande wake wale waliopigwa kikumbo katika duru ya kwanza. Kiwango cha uitikiaji wa wapiga katika duru hiyo, kitakuwa kigezo muhimu cha nani ataibuka mshindi, amesema mchambuzi huyo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, rtre

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW