Colombia yatangaza makubaliano ya kihistoria ya amani
25 Agosti 2016Pande hizo mbili zimesema zimefikia makubaliano kuhitimisha mgogoro na kujenga amani, katika taarifa ya pamoja iliyosomwa na wawakilishi wa Cuba na Norway, ambao ndiyo wapatanishi katika mazungumzo yaliyopelekea kufikiwa makubaliano hayo.
"Tumefikia makubaliano ya mwisho... kuhitimisha mgogoro na ujenzi wa amani imara na endelevu nchini Colombia," alisema mwakilishi wa Cuba Rodolfo Benitez, akisoma taarifa kabla ya makubaliano hayo kusainiwa na viongozi wa ujumbe wa waasi na serikali.
Makubaliano hayo ya kihistoria yanatazamiwa kulivunja kundi la Revolutionary Armed Forces of Colombia (FARC), ambalo waasi wake waliokuwa wakifadhiliwa na madawa ya kulevya ya cocain, walipigana dhidi ya serikali katika vita vilivyosababisha vifo visivyopungua 220,000. Mamia kwa maelfu wengine walitoweka na mamilioni waliyakimbia makaazi yao kwa sababu ya vurugu.
Akizungumza mapema nchini Colombia, Rais Juan Manuel Santos alisifu habari hizo za kihistoria. "Kwa bahati nzuri tumeweza kufiki bandari salama," alisema kiongozi wa FARC, Timeleon "Timochenko" Jimenez.
Katika muda wa siku chache zilizopita, serikali na FARC walikuwa wanajadili masuala kadhaa yaliosalia bila kutatuliwa, na kufanya kazi hadi usiku wa manane siku ya Jumanne kuandaa muswada wa taarifa ya pamoja, duru kutoka kutoka ujumbe wote zililiambia shirika la habari la AFP mjini Havana.
Paka Colombia ya amani
Rais Santos alitabasamu wakati akizungumzia kile alichokiita "siku maalumu kabisaa". "Naomba nchi hii ambayo mnachora taswira yake na kuipaka iwe kweli," aliliambia kundi la watoto wanaoshiriki mashindano ya uchoraji yanayodhaminiwa na serikali yaliopewa jina la "Paka Colombia katika amani."
Makubaliano hayo yaliopingwa na marais wawili wa zamani wa Colombia, bado yanahitaji kuidhinishwa katika kura ya maoni kabla ya kuwa sheria. Rais Santos amesema ataitisha kura hiyo ya maoni mnamo Oktoba 2 na Alhamisi hii atayawasilisha kwa bunge la Colombia kwa ajili ya kujadiliwa.
Tafiti mbalimbali za maoni zinaonyesha kuwa Wacolombia wengi watayaunga mkono. Lakini licha ya hayo, Santos ambaye ameifanya amani kuwa nguzo ya urithi wake, atalaazimika kupambana ipasavyo kwa ajili ya kura ya ndiyo kutokana na upinzani mkali kutoka kwa sekta zenye nguvu za taifa hilo zinazodhani kuwa suluhu pekee ni kuwasambaratisha FARC kijeshi.
"Kura chanya ilionekana wakati mmoja kama ndoto," alisema Tom Long, mhadhiri wa uhusiano wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha Reading. "Lakini upinzani kutoka kwa marais (Andres) Pastrana na (Alvaro) Uribe utamlazimisha Santos kupiga kampeni ya nguvu kuunga mkono makubaliano."
Duru ya huko nyuma ya mazungumzo chini ya Pastrana kati ya mwaka 1999 na 2002 ilivunjika baada ya waasi kuiteka ndege. Pande mbili zilisaini mapatano ya kusitisha mapigano mwishoni mwa mwezi Juni, ikiwemo miongozo ya namna waasi wa FARC wangeweka chini silaha zao.
Tangu wakati huo mazungumzo yamejikita katika ushiriki wa baadae wa kisiasa wa waasi, kujumuishwa wapiganaji katika jamii ya kiraia, na ufafanuzi juu ya namna jamii ya kimataifa itasimamia utekelezaji wa makubaliano.
Obama apongeza
Rais wa Marekani Barack Obama alizungumza kwa njia ya simu na rais Santos siku ya Jumatano, na kumpongeza kwa kukamilisha mazungumzo hayo.
Ikulu ya White House ilisema katika taarifa kuwa Obama anaitambua siku yalipokamilishwa makubaliano hayo kuwa muhimu katika kile kitakachokuwa mchakato mrefu wa kutekeleza kikamilifu, makubaliano ya haki na ya kudumu, yanayoweza kuhakikisha usalama na mafanikio kwa watu wa Colombia.
Marais hao wawili pia walikubaliana kuendeleza ushirikiano wa karibu na juhudi za pamoja kupambana na uhalifu wa kupanga na usafirishaji wa madawa ya kulevya.
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, pia aliwapongeza Santos, Londono na timu zao za majadiliano kwa juhudi zao na uvumilivu. "Sasa kwa vile makubaliano yamekamilishwa, juhudi sawa na ya kipekee itahitajika kutekeleza makubaliano hayo," alisema msemaji huyo.
Baraka kwa biashara
Makubaliano na FARC hayahakikishi mwisho wa vurugu zilizoanza kama uasi wa wakulima. Mazungumzo kati ya kundi dogo la mrengo wa kushoto la Jeshi la Ukombozi wa Taifa na serikali yalikwama hivi karibuni. Magenge yaliotokana na makundi ya kijeshi ya mrengo wa kulia yanaripotiwa kuziteka baadhi ya njia za FARC za usafirishaji madawa ya kulevya.
Lakini makubaliano ni sharti la amani. Usitishaji mapigano tayari umepelekea kupungua kwa vurugu kwa kiwango cha chini kabisaa katika kipindi cha miongo kadhaa. Hali iliyoboreka ya usalama inapaswa kuchochea uwekezaji na utalii na huenda ikafungua maendeleo katika maeneo ya vijijini, wanasema wachambuzi, wakikadiria ongezeko la ukuaji wa kiuchumi kwa asilimia 0.3 hadi 1.
"Ukiwa na uborekaji jumla katika hali ya usalama, uwekezaji wa kigeni na kitaifa unaongezeka," alisema Sabine Kurtenbach kutoka taasis ya utafiti ya GIGA iloyoko mjini Hamburg, Ujerumani.
Historia ya FARC
Kundi la FARC lilizaliwa kama makundi mengine ya uasi wa kimarx wa wakulima katika Amerika ya Kusini mnamo miaka ya 1960, kutokana na kuvunjwa moyo na ukosefu wa usawa na kiuchumi na kijamii.
Likifadhiliwa na madawa ya cocain na utekaji nyara kwa ajili ya fidia, kundi hilo lilipanika na kufikisha kikosi cha wapiganaji 17,000 kikiendesha operesheni zake katika maeneo makubwa ya Colombia.
Wakati makundi mengine ya uasi ya Amerika Kusini yalisambaratishwa na serikali za mrengo wa kulia au kushwawishiwa kujiunga na siasa za kawaida kufikia miaka ya 1990, FARC iliendelea kuwa imara.
Walianza kubadilika tu wakati Uribe alipoanzisha kampeni ya kupambana na uasi iliyoungwa mkono na Marekani mnamo mwaka 2002 na kuwauwa viongozi wengi wa FARC na kupunguza wapiganaji wake hadi karibu 7,000.
Uribe anasema serikali inasalimu kwa ugaidi kwa kujiadiliana na FARC na kuipa kiwango cha msamaha. Chama chake, ambacho ndiyo chama kikuu cha upinzani Colombia, kilitangaza mapema mwezi huu kuwa kitaunga mkono upande wa "hapana" katika kura ya maoni.
China ya makubaliano yaliyofikiwa tayari nchini Cuba, watendaji wa uhalifu mbaya zaidi watakabiliwa na "sheria ya mpito" inayolenga zaidi katika kubaini ukweli kuliko kutoa adhabu kali.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe.
Mhariri: Yusra Buwayhid